Wabunge wanne Chadema matatani

16Nov 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Wabunge wanne Chadema matatani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa amri ya kukamatwa wabunge wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufikishwa mahakamani kwa kukiuka masharti ya dhamana akiwamo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Wengine ni Mbunge wa Bunda Mjini , Ester Bulaya, John Heche wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa wa Iringa Mjini ambao wote na wenzao watano wanakabiliwa na mashtaka ya 13 ya uchochezi.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya washtakiwa hao kushindwa kufika mahakamani wakati kesi yao ilipopangwa kuendelea kusikilizwa.

Vigogo hao wa Chadema wameshindwa kufika mahakamani bila kutoa au  kuwapo taarifa kutoka kwao na wadhamini wao.

Awali kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa ushahidi wa mshtakiwa wa kwanza, Mwenyekiti wa Taifa Chadema, Freeman Mbowe, ikiwamo kuhojiwa na mawakili wa Jamhuri.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai kuwa washtakiwa wanne hawako mahakamani na kwamba Jamhuri hawana taarifa, hivyo kuomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Hakimu Simba alisema jana kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa ushahidi wa utetezi kuanzia saa 3:00 asubuhi.

Alisema mahakama yake inatoa hati ya kukamatwa washtakiwa hao wanne kwa kukiuka masharti ya dhamana na kutoa hati ya wito kwa wadhamini wao kwenda kujieleza kwanini hawakuwapeleka washtakiwa kusikiliza kesi yao kama masharti ya dhamana yanavyowaelekeza.

Wakili wa utetezi, Faraji Mangula, alidai ameshika mikoba ya mawakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala na Jeremiah Mtobesya kwamba ana taarifa za Bulaya.

Hata hivyo, Hakimu alimwelekeza Wakili Mangula kwamba mwenye jukumu la kutoa taarifa za mshtakiwa ni mdhamini na si kazi ya wakili.

Wakili Nchimbi aliiomba Mahakama itoe hati ya kuwakamata washtakiwa hao na wito kwa wadhamini wao ili wajieleze kwa nini hawakuwapeleka washtakiwa mahakamani kama masharti ya dhamana yanavyotaka.

Mahakama hiyo iliridhia imetoa amri ya kukamatwa washtakiwa na wito kwa wadhamini, Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa ushahidi wa utetezi  Novemba 19, 20 mpaka 21, mwaka huu.

Washtakiwa waliofika mahakamani  hapo jana ni Mbowe,  Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu,  Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

Katika Kesi hiyo Mbowe na wenzake wanaokabiliwa na  mashtaka 13, ikiwamo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki kwa Watanzania dhidi ya Serikali.

Habari Kubwa