Kilimanjaro Queens morali juu ikiivaa Sudan Chamazi

16Nov 2019
Shufaa Lyimo
Nipashe
Kilimanjaro Queens morali juu ikiivaa Sudan Chamazi

TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens, inashuka dimbani leo dhidi ya Sudan Kusini katika mechi ya ufunguzi wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge) kwa Wanawake-

-ikiwa na lengo moja tu la kulibakisha kombe hilo nchini, kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Bakari Shime.

Akizungumza na Nipashe jana, Shime alisema kikosi hicho kipo vizuri kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Chamazi na kueleza amewapa mazoezi ya kutosha.

"Maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yanaendelea vizuri, wachezaji wote wapo vizuri kila mmoja ana morali ya ushindi," alisema.

Alisema kila mchezaji ameahidi kujituma kuhakikisha kombe hilo linabaki nyumbani, ukizingatia wao ndio wenyeji wa mashindano hayo.

Kocha huyo alisema anaziheshimu timu zote ambazo zinashiriki mashindano hayo kwa kuwa zina viwango vizuri.

Aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu hiyo inapokuwa dimbani ili icheze kwa kujiamini.

Hii ni mara ya tatu, michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kufanyika katika Ukanda huu, ambapo mara ya kwanza ilifanyika 2016 katika mji wa Jinja Uganda na mwaka jana yalifanyika Kigali Rwanda huku Kilimanjaro Queens ikitwaa ubingwa katika kila msimu.

Mwaka huu mashindano hayo yanashirikisha jumla ya nchi nane ambazo ni wenyeji Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), Tanzania visiwani (Zanzibar Queens), Sudan Kusini, Burundi, Uganda, Kenya, Ethiopia pamoja na Djibouti.