Serikali yashtukia upigaji mabilioni ununuzi korosho

18Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Serikali yashtukia upigaji mabilioni ununuzi korosho

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, ameunda timu ya watu wasiozidi watano kwa ajili ya kuhakiki uuzaji na ulipaji wa korosho kwa wakulima katika msimu wa kilimo 2018/19, baada ya kubaini kuwapo na madudu kwenye malipo hayo.

Pia, amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza kiasi cha Sh. bilioni 53.2 kilichobaki kwenye akaunti ya Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza zao la korosho uliofutwa, ambazo zilikuwa kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho na maghala.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Hasunga alisema katika msimu huo serikali ilinunua korosho kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, lakini imebainika kuwapo na madudu mbalimbali ikiwamo malipo hewa, kilo za uongo na wakulima feki huku akiwataka wakulima wanaodai kupeleka madai yao kwa timu hiyo na kamati za ulinzi na usalama.

Alisema timu hiyo itashirikiana na kamati iliyokuwa chini ya wizara hiyo ambayo iliundwa kwa ajili ya kuhakiki ununuzi wa zao hilo na kazi yake itakamilika ifikapo Januari 15, mwaka huu.

Hasunga alisema fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili hiyo zaidi ya Sh. bilioni 700 ni nyingi hivyo kuna umuhimu wa kujiridhisha kama zimewafikia wakulima.

"Tumeunda timu ya watu wasiozidi watano ili kushirikiana na kamati ya wizara iliyokuwa inahakiki, tuhakiki tuwe na uhakika wa korosho zilizopokelewa, ziliouzwa, fedha zilizopatikana na kama kuna upungufu ibaini na tume ihakikishe wote waliolipwa ni wale wanaostahili kulipwa."

"Tuhakikishe majina yaliyotoka kwenye vyama vya msingi kuja kwenye vyama vikuu na walioenda kwenye mfumo wa malipo kwenda benki ya TADB, na kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko mpaka majina yaliyopelekwa kwenye benki, fedha zilizoingia ziliingia kweli kwenye akaunti za wakulima," alisema.

Kadhalika timu hiyo itaangalia kama kunaunyaufu ulijitokeza ili kutoa taarifa yenye uhalisia.

"Tumebaini kuna baadhi ya vyama vya ushirika, pamoja na kwamba kamati za ulinzi na usalama zilihakiki, lakini kuna udanganyifu katika malipo ya wakulima, kutokana na udanganyifu huo tunapata mashaka huenda baadhi ya wakulima waliolipwa sio sahihi," alisema.

Alitoa mfano wa Mkoa wa Pwani katika Chama cha Msingi cha Sangasanga Amcos ambacho alisema kilidanganya kikaonyesha wamekusanya kilo 218,000, lakini kilo halisi ni 212,000.

"Kuna kilo za uongo hapo, lakini walidanganya wakaweka kwamba korosho zilizopatikana zina ubora wa daraja la kwanza wakati kilo 244 zilikuwa hazina ubora huo, malipo hewa kwa baadhi ya watu siyo wakulima, hawakuleta korosho pale kwenye chama cha msingi, lakini majina yao yapo kwenye malipo ya mwisho na wamelipwa," alisema.

Udanganyifu katika ulipaji

Alibainisha kuwa fedha zilizolipwa kwa watu ambao sio wakulima ni Sh. milioni 222.3 kwa chama hicho.

"Hii ni kwa chama hicho kimoja tu, lakini kuna vyama vingine tumepata changamoto ya aina hiyo kule Tandahimba kama isingekuwa uaminifu wa watu waliokuwa wanahakiki kulikuwa na Sh. bilioni 1.6 zilikuwa za udanganyifu, na maeneo mengine kumeonekana na udanganyifu," alisema.

Vile vile, wamebaini baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kwa kushirikiana na viongozi wengine kutoa majina ya uongo na si halisi ya wakulima.

"Kabla ya kumaliza kulipa, na kumaliza msimu tukaona ni vyema tujiridhishe kwanza tani zote zilizopokelewa za korosho kwa vyama vyote kwa msimu huo, ndiyo hizo zote tulizopeleka kwenye mauzo na kama kuna upungufu wa tani nani aliyesababisha ili tuchukue hatua zinazostahili," alisema.

Pia watahakiki majina yanayotoka kwenye vyama vya msingi, wanatakiwa kulipwa kiasi gani kutokana na kilo alizouza ili kujua kama ndiyo waliolipwa.

"Kama sivyo nani kapindisha na wapi ili kuchukua hatua stahiki, pia tunataka kuhakiki kama kuna wakulima ambao hawajalipwa maana natumiwa meseji nyingi kuwa sisi hatujalipwa wakati tumeshatangaza malipo yote tumemaliza, pale Rais alipotoa Sh. bilioni 40 za kumalizia," alisema.

Hasunga alitaka kujua kama kuna mkulima hajalipwa ni nani na kwa sababu gani.

"Tumeona hata kwenye ufuta mnunuzi anazidishiwa kilo kwa makusudi na njama zinafanya na viongozi wa vyama vya ushirika," alisema.

Alifafanua kuwa hadi mwisho wa msimu huo zilikuwa zimekusanywa tani 222,561.2 za korosho ghafi na thamani yake ilikuwa ni Sh. bilioni 723.8.

"Korosho zilikuwa na madaraja tofauti tofauti, daraja la kwanza zilipatikana tani 204,476.1 ambazo zilikuwa na thamani ya Sh. bilioni 674.71, lakini daraja la pili zilipatikana tani 18,084.9, zenye thamani ya Sh. bilioni 47.7."

Kuhusu korosho ambazo zimeshalipwa ni tani 217,786 ambazo zina thamani ya Sh. bilioni 707.8.

"Tumelipa hizi korosho, lakini kuna mambo machache yamejitokeza, kwanza wananchi hawajamalizika kulipwa na azma ya serikali ni kulipa malipo ya wakulima wote."

Vile vile alisema: "Katika kikao cha mwisho tulichokutana na Rais, wakuu wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani kila mmoja aliulizwa ni kiasi gani unachodai wakulima hawajalipwa, kila mmoja alitaja kiwango kinachodaiwa na tukapata takribani Sh. bilioni 40."

Waziri Hasunga alifafanunua kuwa Rais aliruhusu fedha hizo zitolewe kwenda kumalizia malipo ya wakulima, lakini akasema hadi sasa malipo hayo hayajaisha kutokana na mambo machache ambayo yamejitokeza kwwa baadhi ya vyama vya ushirika, pamoja na kwamba kamati za ulinzi na usalama zilihakiki, lakini kuna udanganyifu.

Ukaguzi wa CAG

Waziri Hasunga alisema Desemba mwaka 2016, serikali ilifuta Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza korosho na kwenye akaunti kulikuwa na Sh. bilioni 53.2 zilizokuwa kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho na maghala.

"Kazi nyingine ilikuwa ni kuendeleza zao la korosho, kilichojitokeza Bodi ya Korosho badala ya kutekeleza maagizo ya serikali walikiuka na walibadilisha matumizi," alisema.

Alisema kilichowashtua mwaka huu wakati minada inaendelea, walioagiza magunia wameleta madeni kwamba wanaidai serikali kutokana na kusambaza magunia 2017/18.

"Kuna kampuni inadai Sh. bilioni saba, nyingine bilioni tano, wanasema walisambaza magunia, wakati utaratibu ulikuwa mnunuzi ananunua na kulipia gunia, swali linakuja hizo fedha hazikulipa magunia na kwanini madeni yaje leo."

"Tulipoomba maelezo Bodi wakatuletea matumizi ya fedha zilizobaki kwenye mfuko ya zile Sh. bilioni 53.2, katika fedha hizo walitumia Sh. bilioni 28.1 kununua viuatilifu, kibaya zaidi wanasema wametumia Sh. bilioni 12.2 kununua magunia, sasa swali mnunuzi alikuwa analipia magunia, lakini kama walilipa madeni ya magunia kwanini kuwe na madeni leo, ukiangalia yana kiwango hicho hicho," alisema.

Madudu yabainika

Waziri Hasunga aliendelea kueleza kuwa wameamua kujiridhisha na fedha hizo na matumizi yake kwa kumwagiza CAG kukagua ili serikali ichukue hatua zinazostahili kutokana na kuwapo na madudu kwenye matumizi hayo.

"Kuna fedha zimetolewa kwenda kulipia madeni ya benki ya nyuma kwa vyama vya ushirika, Chama cha Tanecu kilipewa Sh. bilioni 1.87, Koecu kilipewa Sh. bilioni 2.12 kulipia madeni ya nyuma wakati zilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na maghala, kibaya zaidi eti wakati wanasimamia zoezi wamelipana Sh. milioni 638.9 watendaji wa bodi, zingine vikao vya wadau wamelipata fedha nyingi takribani Sh.Bilioni moja kuandaa vikao," alisema.

Hasunga alisema kumekuwa na mwenendo mzuri tangu kuanza kwa minada ya wazi na idadi ya wanunuzi wanaojitokeza ni kubwa huku bei zinaendelea kupanda kutokana na mahitaji makubwa ya korosho.

Habari Kubwa