Mkapa: Utitiri wa vyama hatari kwa demokrasia

18Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mkapa: Utitiri wa vyama hatari kwa demokrasia

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema anaamini kuwapo kwa idadi kubwa ya vyama vya siasa nchini ni hatari kwa demokrasia.

Anaona utitiri wa vyama vya siasa nchi unadhoofisha ushindani, akidokeza kuwa vyama vingi vilivyopo nchini vimeanzishwa kwa maslahi ya wachache badala ya maslahi ya umma.

Mkapa aliyeiongoza Tanzania kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1995, anayasema hayo katika kitabu chake cha 'My Life, My Purpose' (Maisha Yangu, Kusudi Langu).

Rais huyo wa awamu ya tatu anaeleza Tanzania ina vyama vingi vya siasa, lakini vingi vimeanzishwa kwa lengo la wahusika kujinufaisha kiuchumi badala ya kulisaidia taifa.

Anasema baadhi ya vyama havina hata idadi kubwa ya wanachama na muundo wake ni sawa na alichokiita familia.

"Uwapo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia. Watu wanaingia katika siasa kusaka manufaa ya kiuchumi, siyo kwa nia tukufu ya kuwatumikia wananchi," anasema katika kitabu hicho kilichozinduliwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Mkapa anaongeza kuwa hata kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Tanzania ilikuwa na vyama vya siasa zaidi ya 20, lakini ni vitano tu vilivyofanikiwa kupata kura za kuviwezesha kuwa na uwakilishi bungeni.

Katika kitabu chake hicho, Mkapa anaeleza zaidi kuwa zamani Tanzania haikuruhusu wafanyabiashara kujihusisha na siasa, lakini sheria ilipolegezwa, ilitoa mwanya kwa kundi hilo kunufaika.

Anasema wafanyabiashara wengi wametumia mwanya huo kujiingiza kwenye siasa ili kulinda maslahi yao, akieleza kuwa hata bungeni, ni wabunge wachache wanaoingia kwenye chombo hicho kutetea wananchi.

Mkapa anasema nchi inakabiliwa na kikwazo cha wabunge na wasomi wake wengi kuhangaika kusaka fursa za posho na safari za nje badala ya kusaidia taifa lao.

Habari Kubwa