Mpina aizindua ajenda ya kitaifa utafiti wa mifugo

18Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Mpina aizindua ajenda ya kitaifa utafiti wa mifugo

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amezindua ajenda ya kitaifa ya utafiti wa mifugo, uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ya mwaka 2020-2025 na kutangaza kuzifumua na kuziibua tafiti zote  zilizofanywa na wasomi na kutelekezwa kwenye makabati miaka ya nyuma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ajenda ya Kitaifa za Utafiti wa Mifugo, Uvuvi na Ukuzaji wa Viumbe Maji ya mwaka 2020-2025 katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mjini Morogoro. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Kutokana na hali hiyo, zitaingizwa kwenye mfumo rasmi wa matumizi ili kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo.

Pia agenda hizo zitaleta msisimko mpya wa kufanya utafiti nchini na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo tafiti nyingi zilifanywa na kutelekezwa kwenye makabati na watafiti mbalimbali wakiwamo Wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu (PHD) katika vyuo vikuu mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ajenda hizo kitaifa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA),  Kampasi ya Mazimbu mjini Morogoro, Waziri Mpina aliziagiza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kubadilika ili kufanya tafiti kwa vigezo vilivyowekwa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta za mifugo na uvuvi nchini.

Waziri Mpina alisema chimbuko la kuandaliwa kwa ajenda hizo za utafiti ni baada ya kubaini kuwa ajenda zilizokuwapo awali za mifugo na uvuvi zilishindwa kuibua na kuzitumia tafiti zilizofanywa kuchochea mabadiliko kwenye sekta hiyo muhimu ya uzalishaji.

Pia ajenda za utafiti zilizokuwapo za mifugo na uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti zinazofanywa na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu, lakini sasa ajenda za utafiti zilizozinduliwa zimeweka utaratibu wa namna ya kuzitambua, kuziorodhesha na kuzitumia tafiti za wasomi hao.

“Haiwezekani tafiti za wasomi wa kiwango cha juu kiasi hicho wanazozifanya wakati wa kukamilisha masomo yao ziishie kupata alama za ufaulu na kutupwa kwenye makabati, leo kila mhitimu atalazimika kuandaa ‘policy brief’ ambayo itawezesha watumiaji na serikali kurekebisha au kuandaa sera na sheria,” alisema Waziri Mpina.

Aliongeza kuwa ajenda za utafiti zilizokuwapo za mifugo na uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuweka kanuni ambazo zitahakikisha kuwa utekelezaji  wa ajenda za utafiti unafanyika, lakini ajenda za utafiti iliyotangazwa inaweka kanuni zitakazotoa mwongozo na usimamizi wa utekelezaji na wajibu wa kila mhusika.

Aidha, Waziri Mpina alibainisha kuwa ajenda za utafiti zilizokuwapo za mifugo na uvuvi hazikuwa na utaratibu wa kuwaunganisha watafiti wa mifugo na uvuvi nchini, na hivyo kupelekea kila mmoja kufanya utafiti kivyake hali iliyosababisha jambo moja kufanyiwa utafiti na mtafiti zaidi ya mmoja na kukosa jukwaa la kuratibu na kuchambua tafiti zinazofanywa nchini.

“Ajenda ninayoizindua leo inakwenda kujumuisha watafiti na wataalamu mbalimbali waliobobea katika fani za mifugo, uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji ili kuyapitia matokeo ya utafiti, teknolojia zilizoibuliwa na utafiti na kuzisambaza kwa watumiaji kwa manufaa ya Taifa,” alisema Waziri Mpina.

Pia Waziri Mpina alibainisha upungufu mwingine uliyomo kwenye ajenda za utafiti zilizokuwapo za mifugo na uvuvi ni pamoja na kutoweka msingi mzuri wa kusimamia watafiti na kufanya tafiti kulingana na mahitaji ya soko badala yake  taasisi za utafiti na watafiti kufanya tafiti nyingi za nje na mambo muhimu ya wananchi yanayohitaji kufanyiwa utafiti kutelekezwa.

Habari Kubwa