Msako waanza wanaodaiwa kuchoma shamba la Mzindakaya

18Nov 2019
Gurian Adolf
NKASI
Nipashe
Msako waanza wanaodaiwa kuchoma shamba la Mzindakaya

SERIKALI wilayani Nkasi mkoani Rukwa imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watu waliowashawishi wakazi wa kijiji cha Nkundi kuchoma shamba la mwekezaji na mwanasiasa mkongwe, Chrisanti Mzindakaya, na kusababisha hasara ya Sh. milioni 95.

Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mtanda, wakati akizungumza na wakazi wa kijiji hicho alipokwenda kushuhudia tukio hilo.

Alisema shamba hilo ni mali ya Mzindakaya na analimiliki kisheria hivyo wananchi wasijidanganye kuwa wanaweza wakamnyang'anya kwa nguvu na kuwataka wafuate taratibu za kisheria.

"Kitendo cha kuchoma shamba kimefanywa na wananchi wachache katika kijiji hicho, hivyo ninaliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wote pamoja na watu wanaowashawishi kufanya hivyo ili sheria ichukue mkondo wake, na wakae wakijua kuwa serikali ya wilaya haipo tayari kuona wawekezaji wanahujumiwa, kama wananchi wana madai wafuate taratibu za kisheria," alisema.

Alieleza kuwa akiwa mlinzi wa amani amebaini migogoro inayotokea mara kwa mara na baina ya wananchi wa kijiji hicho na mwekezaji huyo inatokana na baadhi ya watu kuwatia hasira wananchi, kwenda kuvamia shamba la Mzindakaya na kufanya uhalifu wakiwaaminisha kuwa kwa kufanya hivyo watapewa shamba hilo jambo ambalo haliwezekani.

Katika mkutano huo baadhi ya wananchi, Apolinary Msuku na Jofrey Mashauri walimwomba mwekezaji huyo eneo la shamba, ili wananchi wapate ardhi ya kulima kwa kuwa hawana maeneo ya kulima ndiyo maana wamekuwa wakitumia nguvu bila ya kujua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Naye diwani wa kata hiyo, Karasi Kipeta, alisema mwekezaji kwa upande wake alishawaambia kuwa wanaotaka kulima shamba hilo wajiorodheshe ili wakamwombe maeneo ya kulima na atawapatia, lakini wananchi hawataki wanachotaka ni kujimilikisha shamba hilo.

Shamba la Nkundi ambalo lilikuwa ranchi ya taifa lenye ukubwa wa hekta 6,000, aliuziwa Mzindakaya na linazungukwa na vijiji saba vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pamoja Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, wananchi wa vijiji hivyo wanadaiwa kufanya vitendo vya hujuma ili mwekezaji huyo alirudishe na wapewe maeneo ya kulima.

Habari Kubwa