TRA yafikia zaidi ya wafanyabiashara 700

18Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
TRA yafikia zaidi ya wafanyabiashara 700

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewafikia na kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara 700 kupitia kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi iliyofanyika mkoani hapa.

Lengo la kampeni hiyo ilikuwa ni kutoa elimu kuhusu masuala ya kodi pamoja na kusikiliza malalamiko, changamoto na maoni kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo mwishoni mwa wiki, Ofisa Msimamizi wa Kodi Mkuu wa TRA, Julius Mjenga, alisema mamlaka hiyo ililenga kuwafikia wafanyabiashara 500, lakini mwitikio wa watu umefanikiwa TRA kuvuka lengo hilo na kuwafikia zaidi ya 700.

“Wiki hii moja ya elimu kwa mlipakodi, tuliwalenga wafanyabiashara wa wilayani, kumekuwa na changamoto ya kutokupata elimu ya kodi kwa wakati. Nashukuru tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu tumewaelimisha wafanyabiashara 774 katika kampeni hii,” alisema Mjenga.

“Tumefika karibu wilaya zote za mkoa huu wa Morogoro ambazo ni Malinyi, Ulanga, Kilosa, Mvomero, Kilombero na Gairo na kila mahali tulipopita tumepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi mbalimbali.”

Kwa upande wa wafanyabiashara waliotembelewa na TRA, wameishukuru mamlaka hiyo kwa kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi na kuomba elimu hiyo iwe endelevu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara hao walisema, TRA ya sasa siyo ile ya zamani kwa sababu sasa hivi maofisa wake wako karibu na walipakodi na hawana tabia ya kufunga biashara zao.

“Zamani mtu alikuwa akisikia watu wa TRA wanakuja, anafunga duka anaondoka, lakini siku hizi, TRA wamekuwa marafiki, wanatuelimisha na wala hawafungi biashara zetu, kwa kweli tunashukuru sana,” alisema Eleonora Kisimba, mfanyabiashara wa duka la nguo wa wilayani Mvomero.

Naye Stanphord Mjumbe, mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi wilayani Gairo, alisema kampeni ya elimu kwa mlipakodi ifanyike mara kwa mara kwa sababu wafanyabiashara wengi hususani wadogo hawajasoma hivyo wanahitaji kuelimishwa zaidi haki na wajibu wao katika ulipaji kodi.

Wafanyabiashara hao pia wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania kurejesha kodi ya zuio kwa wamiliki wa majengo kwa kuwa baadhi yao hawataki wapangaji kuzuia asimilia kumi na kuiwasilisha TRA.

Vilevile, wameomba kuelimishwa jinsi ya kulipa kodi ya mapato kwa awamu mara tu wanapokadiriwa kodi hususani kwa wafanyabiashara wapya kwa kuwa wengi wao wanapitiliza tarehe za kulipa kodi hiyo kwa kukosa uelewa.

Kampeni ya huduma na elimu kwa mlipakodi imemalizika jana na ilifanyika katika mikoa ya Morogoro na Pwani kwa wafanyabiashara kupata fursa ya kutembelewa katika maduka yao na wengine kuhudhuria semina kwa ajili ya kuelimishwa masuala mbalimbali yanayohusu kodi.

Habari Kubwa