TGNP yawapa ilani wadau wa uchaguzi

18Nov 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
TGNP yawapa ilani wadau wa uchaguzi

WADAU wa uchaguzi na uongozi  juu ya nafasi ya mwanamke katika uchaguzi, wamekutana kujadili kwa kina jinsi ya kumwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika chaguzi mbalimbali.

Uchaguzi unaolengwa ni wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ambao mwanamke naye anatakiwa kuwania nafasi ya uongozi na kuchaguliwa bila kuwekewa mizengwe.

Mkutano wa kujadili suala hilo, ulifanyika Dar es Salaam juzi, ukisimamiwa na  Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), ushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Wadu wengine walikuwa ni wawakilishi wa vyama vya siasa, Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ulingo wa Wanawake na Siasa.

Mbali na hao, wadau wengine katika mkutano huo walikuwa ni Mtandao wa Wanawake na Katiba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec).

Akitoa neno katika mkutano huo, Mkurugenzi wa TGNP, Lilian Lihundi, alisema, Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019, na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Alisema, TGNP imeandaa Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake inayohusu chaguzi hizo, ikilenga kutoa sauti za pamoja za wanawake na makundi mbalimbali (wanawake na wanaume), katika uwezeshaji wa wanawake kushiriki kikamilifu kwenye mchakato mzima wa uchaguzi na kuhakikisha ajenda yao inapewa kipaumbele katika mipango ya serikali inayopewa rdhaa.

"Chaguzi hizi zinafayika kukiwa na historia iliyowekwa katika nchi kwa kupata kwa mara ya kwanza Makamu wa Rais mwanamke (Mama Samia Suluhu Hassan) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na mgombea mwanamke katika nafasi ya urais (Mama Anna Mghwira)," alisema Lihundi.

Alisema, chaguzi hizo zina umuhimu mkubwa kihistoria, katika harakati za ukombozi wa mwanamke kimapinduzi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla, ndiyo maana TGNP ikaanda Ilani hiyo iweze kutoa mchango.

"Ilani hii ni nyenzo muhimu kwa wapigakura wakati wa kusikiliza wagombea wanapojinadi iwapo wamebeba madai haya au la, pia itatumika kuuliza maswali wakati wa kampeni na nyenzo muhimu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa ahadi za wagombea vyama na serikali watakapoingia madarakani," alisema.

Katika mkutano huo, wadau walijadili mikakati ya kufanikisha chaguzi hizo, lakini baadhi wakidai kuonewa na Jeshi la Polisi, rushwa, ubaguzi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Zahra Ali Hamad ni Naibu Katibu Ngombe ya Wanawake CUF, Zanzibar, ambaye alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi bila upendeleo na kukumbusha kuwa bila utawala bora hakuna maendeleo.

"Waache uwanja wa kufanya siasa uwe tambarare badala ya kuegemea upande mmoja wakati nchi hii ni yetu sote na tunatakiwa kuijenga kwa kushirikiana bila upendeleo wowote," alisema Zahra.

Naye mwanaharakati, Gemma Akilimali, alisema umefika wakati sasa wanawake kuchagua wanawake wenzao wanaowania uongozi bila kuangalia vyama wanavyotoka, ili mradi wawe na uwezo wa kuongoza.

Kwa upande wake mwakilishi wa IGP, Inspekta Issa Asali, aliwataka wadau hao kufanya shughuli zao, ajenda ya kwanza iwe ni usalama, kwa vile usalama, amani na utulivu vikikosekana, hakuna ustawi wa jamii.

"Tusitake mambo yaharibike ndipo tuonyoosheane vidole, hivyo hata nyie asasi za kiraia, katika mikutano yenu shirikisheni askari wetu, wapo nchi nzima," alisema Inspekta Asali.

Akizungumzia rushwa ikiwamo ya ngono, mwalikishi kutoka PCCB, Mercy Manyalika aliwataka Watanzania waelewe uthamani wa kura zao kuliko vitu wanavyopokea na kuweka madarakani viongozi wabovu.

"Kwa wale wote watakaombana na kadhia hiyo ya rushwa wapige simu namba 113 wakiwa sehemu yoyote nchini, PCCB itachukua hatua haraka iwezekanavyo," alisema Mercy.Naye Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mathew Mwaimu, aliwataka wadau wote watakaokumbana na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, watoe taarifa.

Habari Kubwa