Tunaishangilia wote Stars, ikipoteza tuwe wote pia

18Nov 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Tunaishangilia wote Stars, ikipoteza tuwe wote pia

ILIKUWA ni siku ya furaha sana kwa Watanzania baada ya kuwachapa Equatorial Guinea mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ijumaa usiku, watu walitoka kwa hoi hoi na nderemo uwanjani mpaka majumbani kwao. Kwenye vibanda umiza nako kulilipuka shangwe kwa mashabiki wa soka kuishangilia timu yao ya taifa.

Kuna abiria waliokuwa kwenye mabasi na magari madogo waliokuwa wakitoka kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, wengine kazini, wakirejea majumbani kwao usiku huo nao wakiwa wanasikiliza matangazo ya mechi hizo kwenye redio walionekana kulipuka kwa sauti za kushamgulia na vigelegele kwa kinamama. Kila Mbongo alifurahi. Watu waliongea lugha moja. Hakukuwa na Usimba, Uyanga wala Uazam. Huu ndiyo ule uzalendo uliokuwa unatakiwa na kuhimizwa tangu mwanzo.

Uzalendo huu unatakiwa udumishwe na kuendelezwa kwa mechi zingine zinazofuata bila kujali matokeo.

Tatizo kuna baadhi ya Wabongo ambao ni wengi, wana tabia ya kuwa vigeugeu. Stars inaposhinda kila kitu kinakuwa sawa na cha wote. Hakuna mtu anayetoa makosa, wala kulalamika kuwa kulikuwa na tatizo sehemu fulani. Ni kwa sababu tu timu imeshinda kama hivi sasa.

Kesho Stars itakipiga na Libya nchini Tunisia kwenye mwendelezo wa michuano hiyo hiyo ya kutafuta tiketi ya kufuzu Afcon nchini Cameroon mwaka 2021.

Tukishinda kama wote tunavyoombea furaha zitaendelea kwa Watanzania wote. Lakini itakapotokea kupata sare au kufungwa tatizo litaanza. Wabongo tutaanza kugeukana.

Kwanza huko mitaani na kwenye mitandao ya kijamii ndiyo balaa mara nyingi litakapoanzia. Utaanza kusikia iliyofungwa siyo timu ya taifa ni timu fulani kwa sababu tu ina wachezaji wengi wa klabu hiyo.

Wengine watasema timu haikushinda kwa sababu mchezaji fulani na fulani hawakuchanguliwa kwenye kikosi hicho.

Baadhi watasikika hata kwenye redio wakimponda Juma Kaseja kuwa si kipa, badala yake arudishwe Aishi Manula. Na hili lilianza baada ya kufungwa bao la kwanza dhidi ya Equatorial Guinea, ila limefutika baada ya ushindi.

Bado kuna wale watakaosema kuwa Kocha Etienne Ndayiragije hafai. Tatizo la Wabongo wengi timu inapokuwa haifanyi vema basi kila mmoja anakuwa kocha. Haikatazwi kutoa maoni, lakini yawe ya kujenga, na si ya kuzidi kuwachanganya watu na wasijue la kufanya.

Timu inapokuwa haifanyi vizuri maoni yaonekane kuwa ya ushauri zaidi kuliko kulaumu, na hii italisaidia sana hata Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuchukua ushauri na kuufanyia kazi.

Kama ambavyo kwa sasa tupo pamoja kwenye furaha ya ushindi, ikitokea kwa bahati mbaya kama Stars haikufanya vizuri Wabongo tuwe wote kwenye huzuni.

Tushangilie na kuhuzunika pamoja huku tukitoa maoni ya nini kifanyike badala ya lawama zisizo na kichwa wala miguu na zisizotatulika.

Habari Kubwa