Pengo amtabiria makubwa Makonda

19Nov 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Pengo amtabiria makubwa Makonda

ASKOFU Mkuu Mstaafu wa kanisa katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, amesema anafurahishwa na utendaji wa Paul Makonda na anaona Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam anafaa kurithi mikoba ya Rais John Magufuli.

Pengo (75), aliyasema hayo jana katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa dini na Makonda kuzungumzia mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli katika jiji hilo.

Alisema kama wakiwapo vijana wengi wanaomsaidia kazi Rais Magufuli mfano wa Makonda, ni wazi kuwa hakutakuwa na haja ya kufikiria nani ataendeleza kazi nzuri zinazofanywa na Rais huyo.

 “Tunajiuliza baada ya Magufuli atakuwapo nani, mkiwapo kama wa aina yako (Makonda) wengi, mimi nisingekuwa na shaka kwamba tungekuwa na watu gani wa kuendeleza kazi za Magufuli," alisema Kardinali Pengo.

Kiongozi huyo wa kiroho pia alisifu kazi aliyodai ni nzuri ya Makonda kueleza miradi inayotekelezwa na serikali, akifafanua kuwa Mkuu wa Mkoa huyo ameonyesha ni aina gani ya kiongozi anayemsaidia Rais Magufuli.

“Makonda asante kwa kuniita, katika uzee niliyonao, ningekuwa nimechoka kukaa saa mbili ulizokuwa unaelezea kazi zinazofanywa na serikali, lakini sikuchoka hata katika hali yangu ya uzee. Na hata ongeongeza saa nyingine moja ningekuwapo bila kukuomba ruhusa ya kutoka nje," alisema.

Kardinali Pengo alidai Makonda ni moja kati ya wasaidizi bora walio pembeni ya Rais Magufuli na wanapomwombea aendelee, wanaombea na vijana wa aina yake waendelee.

"Na tunamwomba Mwenyezi Mungu atujalie viongozi wa aina yako wengi zaidi. Kwa maana hii Rais ni mtendaji kazi, lakini hawezi kufanya yote peke yake, anahitaji watu chini, juu na pembeni yake ambao wapo naye kwa ajili ya kumsaidia," alisema.

Kardinali Pengo pia alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi anazozifanya tangu aingie madarakani na kuwashangaa watu aliodai wanamwita dikteta.

“Katika mitandao kumezuka maneno kwamba Rais wetu ni dikteta. Yale anayoyafanya anashughulikia kuendeleza vitu kuliko kuendeleza watu.

"Wanaongelea juu ya kushughulikia vitu kuliko watu ni watu gani hao hawajashughulikiwa wakati mambo mengi yanafanyika kwa ajili ya watu?

“Ni lugha ambayo kwa akili zangu za kizee, siwezi kuelewa, utakuwa unamshughulikia mtu kiasi gani kama unamfanya mtoto wake na mjukuu wake waende shule?" alihoji Pengo.

Awali, Makonda alisema kasi ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo inayofanywa na Rais Magufuli, inazidi maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Kawafanya hata viongozi wa serikali wanaotumia hirizi kumtaja Mungu kwanza. Mara nyingi ameweka wazi kuwa mambo yanavyokwenda kasi hata yeye mwenyewe anamshangaa Mungu," alisema.

Makonda alisema katika kukabiliana na tatizo la utiririshaji wa majitaka, Mkoa wa Dar es Salaam, yuko kwenye mpango wa kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya kuchakata maji taka na kuyarudisha kwenye matumizi.

Alikumbusha mpango wa kujenga kituo eneo la Jangwani na kitagharimu Sh. bilioni 800. Kituo hicho kinatarajiwa kukusanya majitaka kutoka maeneo ya Kariakoo, Upanga, Posta na mitaa mingine ya katikati ya jiji hilo.

Katika mkutano huo, Makonda aliwaomba viongozi wa dini kuwakumbusha waumini wao kuwaheshimu watu walioapa kulinda nchi na usalama wao.

Alisema Jeshi la Polisi na majeshi mengine yanafanya kazi kubwa kuhakikisha mkoa unakuwa na amani huku ulinzi na usalama vikitawala.

“Kulikuwa na ujambazi zamani, watu walikuwa wanauawa ovyo, wakati mwingine hata polisi walikuwa wanashambuliwa, lakini sasa kazi kubwa imefanyika, kuna utulivu, hakuna panya roads wala wizi wa vifaa vya magari,” alisema.

“Mikakati mingi iliwekwa na (Lazaro) Mambosasa (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) na wenzake na matokeo tunayaona jiji la Dar sasa ni shwari," Makonda alitamba.