Mkapa ashtushwa na kasi ongezeko la watu

19Nov 2019
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Mkapa ashtushwa na kasi ongezeko la watu

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa amesema ongezeko la watu ni tishio kwa maendeleo ya nchi, akishauri kuwe na sera madhubuti ili kulikabili.

Katika kitabu chake cha 'My Life, My Purpose' (Maisha Yangu, Kusudio Langu), kilichozinduliwa na Rais John Magufuli jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkapa anagusia hoja hiyo akieleza shaka yake kuhusiana na kasi ya ongezeko la watu nchini.

Anasema anasikitika kuona suala hilo ni tatizo kubwa si tu Tanzania, bali bara la Afrika kwa ujumla huku kukikosekana mjadala wa kutafuta ufumbuzi wake.Mkapa aliyeiongoza Tanzania kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1995, anasema katika kitabu hicho kuwa haoni sera na mwongozo sahihi wa kuikabili ishara hiyo mbaya kwa maendeleo ya umma.

"Ongezeko la watu katika nchi siyo kipimo cha maendeleo bali ni kikwazo kwa maendeleo. Shida kubwa ya nchi nyingi za Kiafrika hatuna mjadala madhubuti kuhusu sera ya idadi ya watu katika nchi zetu," Mkapa analalamika.

Kiongozi huyo mstaafu anaeleza ubashiri wa kisayansi wa mwelekeo wa sensa zijazo, kwamba ifakapo mwaka 2025, ambao ndiyo ukomo wa Dira ya Maendeleo ya Taifa, nchi inatarajiwa kuwa na wakazi milioni 67. Tanzania ina eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 947,300.

Juni 1999, Tanzania ilizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo pamoja na mambo mengine, inalenga kupunguza nusu ya watu wanaoishi katika umaskini na kuwafanya wawe katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mkapa anabainisha kuwa wakati wa uhuru mwaka 1961, kulikadiriwa kuwapo Watanganyika milioni 10.4 na idadi iliongezeka hadi milioni 27.4 alipoanza kukalia kiti cha urais mwaka 1995 na iliongezeka hadi milioni 36.1 wakati anaondoka mwaka 2005.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania mwaka huu, inakadiriwa kuwa na watu 55,890,747 (milioni 55.89). Kati yao, wanaume ni 27,356,189 na wanawake 28,534,558.

Kwa makadirio hayo, idadi imeongezeka kwa watu milioni 43.59 katika kipindi cha miaka 42 kwa kuwa takwimu za NBS zinaonyesha mwaka 1967, Tanzania ilikuwa na watu milioni 12.3, Tanzania Bara ikiwa na watu milioni 11.9 na Zanzibar watu 354,815.

Vilevile, Ripoti ya Juni 21, 2017 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA), ilibainisha kuwa Tanzania imo katika nchi tisa zinazochangia kasi ya ongezeko la watu duniani. Tanzania ilitangazwa kuwa ni ya nne barani Afrika.

Ripoti hiyo inaitaja India, taifa linalokadiriwa kuwa na watu bilioni 1.3, ndiyo ya kwanza kwa kasi kubwa ya ongezeko la watu na katika mataifa nane yanayofuata, matano ni ya barani Afrika na matatu ni ya kusini mwa Jangwa la Sahara na mawili ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Orodha ya mataifa hayo kwa nafasi zake nyuma ya India ni Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Pakistan, Ethiopia; Tanzania; Marekani; Uganda na Indonesia.

Vilevile, ripoti inasema wakazi wa dunia wataongezeka kutoka bilioni 7.6 wa mwaka 2016 hadi bilioni 8.6 ifikapo mwaka 2030 ambao ni ukomo wa kipindi cha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG).

SENSA TANZANIA

Mwaka    Idadi ya watu     Tanzania Bara   Zanzibar

1967        12,313,469        11,958,654        354,8151978        17,512,610        17,512,610        476,1111988        23,095,878        22,455,193        640,6852002        34,569,232        33,584,607        984,6252012        44,928,923        43,625,354        1,303,569Chanzo: Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)