Anyongwa kwa kamba ya viatu

19Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
MWANZA
Nipashe
Anyongwa kwa kamba ya viatu

MTOTO Andrea Sekei mwenye umri wa miaka saba, ameuawa kwa kunyongwa na kamba ya viatu na watu wasiojulikana wakati akichunga mbuzi, kondoo na ndama eneo la Mahiringa wilayani Magu mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro

Baba mzazi wa mtoto huyo, Sekei Andrea, mkazi wa kitongoji cha Mahiringa, kijiji cha Isangijo, alisema Jumamosi asubuhi, Andrea alipeleka wanyama hao malishoni na ilipofika saa tano kama ilivyo kawaida yake kuwarudisha nyumbani kwa ajili ya kunywa maji, hawakurudi.

"Nilianza kushtuka saa 5:00 nikasema vipi mbona huyu leo haleti mapema mifugo, kwanini? Nilipofika nikaja kwangu hapa kuna mkubwa wake nikamwambia aende akamwangalie kule anakochungia. Akaenda akaanza kuzungukazunguka lakini hakumuona.

Muda kidogo nikasema nenda sasa hivi au mama yako ukamwambie na huyo Vero wapitie njia nyingine nami nipitie hapa twende tukamtafute. Tukaanza kutafuta mpaka huko nikapata kondoo mmoja.

Nikakutana na wachungaji wengine nikaanza kuwaeleza wakasema muda wa saa tatu saa nne alikuwa anachungia pale mbugani, lakini walimkosa na walimkuta huyo kondoo tu,” alisema.

Sekei alisema kuwa baada ya kumtafuta kwa muda bila mafanikio, walishauriana kuwa wengine waende mnadani Igoma kumtafuta na ilipofika saa 12:00 jioni wakiwa kule mnadani, walipigiwa simu kuwa mtoto ameshaonekana lakini amefariki dunia.

"Ninaiomba serikali ifanye mchakato wapatikane hao watu waliofanya hili tukio la kumnyonga mtu mpaka kufa," alisema Sekei.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahiringa, Balekele Balele, alisema watuhumiwa waliotenda kosa hilo la kinyama waliondoka na mbuzi na kondoo zaidi ya 50 aliokuwa akiwachunga mtoto huyo.

"Taarifa za kutoonekana mtoto nilipokea nikiwa msibani Kisesa, nikasema kitu cha kwanza baba mzazi wa mtoto aje na mwanazengo mmoja twende kituo cha polisi tutoe taarifa halafu tuongeze jitahada za kutafuta tukishirikiana na Jeshi la Polisi.

Saa 11 jioni walikuja tukaenda polisi, mwenyekiti wa kijiji na baba mtoto kwa mawazo ya haraka haraka ikabidi wakimbie machinjioni kwamba labda wale mbuzi wamepelekwa machinjioni kwenda kuuzwa.

"Tukiwa barabarani kwenda eneo ulipopatikana mwili wa mtoto, tulipata simu kuwa kuna watu wawili wamekutana na wapeleka maziwa Kanyama kwenye mteremko wanaswaga kundi la mbuzi na kondoo wanakimbia sana, pale pale ikabidi tufanye mawasiliano na askari kufuatilia lakini hatukufanikiwa," alisema Balele.

Balele alisema baada ya kuchukua mwili wa mtoto, waliupeleka kituo cha afya Kisesa ambako uchunguzi wa daktari ulionyesha kuwa mtoto alinyongwa kwa kutumia kamba ya viatu.

"Alinyongwa kabisa yaani koromeo lote lilikuwa limekatwa halafu sehemu ya uso hapa alikuwa amepigwa na kitu kizito alikuwa na majeraha damu zinavuja ndicho kitu kilichosababisha mtoto kufa," alisema.

Balele alisema jitihada zinazofanyika sasa ni kuwatafuta hao wahalifu waliofanya tukio la kinyama na kuchukua mifugo.

Diwani wa Bukandwe, Marco Minzi, akitoa neno katika mazishi ya mtoto huyo yaliyofanyika nyumbani kwa wazazi wake, aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi ili kubaini waliofanya tukio hilo.

"Ndugu zangu haiwezekani mtu mgeni kutoka mbali akaja akafanya tukio kama hili bila mwenyeji. Haiwezekani hata siku moja, kama ni mtu ametoka Tarime au ametoka Shinyanga kuja kufanya tukio kama hili, alijuaje kuwa hao mbuzi anachunga mtoto mdogo na kaenda sehemu fulani. Lazima tuumie, tukiumia tukapata ujasiri wa kuwabaini watu waliofanya hivi,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba taarifa hizo ziko kwenye mtandao wa kijamii wa polisi.

Habari Kubwa