Kili Queens raha, Z'bar Queens aibu

19Nov 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kili Queens raha, Z'bar Queens aibu

MABINGWA watetezi wa Kombe la Chalenji kwa Wanawake, Kilimajaro Queens, wameendelea kutoa vipigo kwenye michuano hiyo, na ilikuwa ni zamu ya Burundi kuchapwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Kabla ya mechi hiyo, Kilimanjaro Queens ilitoa dozi ya mabao 9-0 dhidi ya Sudan Kusini Jumamosi iliyopita wakati ndugu zao Zanzibar Queens wakiendeleza aibu kwa kuchapwa tena mabao 5-0 dhidi ya Sudan Kusini baada ya mchezo wa ufunguzi kupigwa idadi hiyo ya mabao na Burundi.

Kwa matokeo hayo, Kilimanjaro Queens imetinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayoshirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Ilikuwa ni dakika ya 34, Kilimanjaro Queens ilipopata bao la kwanza likifungwa na winga wa kushoto, Minja alipotanguliziwa mpira na kuwachomoka mabeki, huku kipa akiwa ametoka goli kumfuata. Kabla hajamfikia, alipiga shuti dhaifu lakini kwa ustadi wa hali ya juu na kujaa wavuni.

Donisia alifunga bao la pili dakika ya 75, Asha Mwalala akafunga bao la tatu dakika ya 75, kabla ya Mwanahamisi kuhitimisha ushindi dakika ya 86.

Kwa upande wa mechi ya Zanzibar Queens, mabao ya Sudan Kusini ambayo kwenye mechi ya kwanza ilichapwa 9-0 na Kilimanjaro Queens, yalifungwa na Amy Lasu, Suzy Iriamba, Aluel Garang', huku Mwajuma Abdallah akijifunga.

Habari Kubwa