Vijana siasa hizi haziwi aina hii

20Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Vijana siasa hizi haziwi aina hii

VIJANA ni wadau muhimu katika shughuli zote za kisiasa na maendeleo ya jamii, kutokana na ukweli kwamba wana nguvu na wepesi wanapotumwa katika kutekeleza majukumu, kuliko watu wazima.

Kwa kutambua hilo, wimbi la mageuzi ya kisiasa lilipoibuka mwanzoni mwa miaka ya 1990, katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Tanzania, baadhi yao walijitosa katika siasa.

Hatua hiyo ni tofauti na miaka ya nyuma, kwani enzi hizo idadi ya watu wanalioshika nafasi mbalimbali kwenye siasa walikuwa ni watu wenye umri mkubwa, lakini sasa hali imebadilika kufuatia vijana kujitosa huko.

Lakini pamoja na vijana kujitosa, kumewapo ushauri, ambao umekuwa ukitolewa na watu wa kada mbalimbali wakiwataka wasitumike vibaya, katika uchaguzi.

Badala yake wawe mstari wa mbele kuhimiza amani, kwa kuzingatia kwamba wao ndiyo wanaotarajiwa kuwa viongozi wa taifa la kesho, hivyo hawana budi kutumika vizuri.

Kama kweli huwa wanatumika vibaya kwa maslahi ya watu wachache, basi ni vyema sasa wakajiepusha na siasa za aina hiyo, kwani vijana wao ndiyo wanaotegemewa kuwa viongozi wa baadaye.

Siyo vizuri vijana kutumika kufanya vurugu za aina yoyote iwe katika uchaguzi au eneo jingine lolote, bali waandaliwe kuwa viongozi wa taifa la kesho na kuepuka kujiingiza kwenye mambo yasiyofaa.

Tayari ipo kwenye mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa nchini mwaka 1992, hivyo vijana wanatakiwa kushindana kwa hoja, huku wakiandaliwa kuongoza nchi, kuliko kutumika vibaya kwenye siasa.

Nikirejea kwenye hoja yangu ni kwamba kampeni za uchaguzi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa zinaendelea, na Watanzania wanatarajia kuchagua viongozi Jumapili ijayo.

Uchaguzi huo utafanyika kukiwa na sintofahamu, kufuatia baadhi ya vyama vya upinzani kuususia, vikitoa sababu mbalimbali, ikiwamo kutoridhishwa na mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uongozi.Pamoja na sintofahamu hiyo, serikali imeshaweka wazi kwamba haimlazimishi wala kumshinikiza mtu yeyote kwenda kupiga kura katika uchaguzi huo.Kwa upande mwingine ni kwamba asiwapo mtu wa kumzuia mwenzake asiyende kupiga kura, eti kwa sababu chama chake kimesusia uchaguzi huo, bali kila Mtanzania awe huru kushiriki au kutoshiriki.Bahati mbaya vijana ndiyo huwa wanadaiwa kutumika katika mchezo huo, ni vyema sasa watafakari kwa umakini na kuacha kutumiwa na wanasiasa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.Ni vyema kuzingatia kile kilichosemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwamba jambo la msingi ni kuhakikisha ulinzi, usalama, utulivu na amani  vinakuwapo siku ya kupiga kura, na hakuna atakayeshinikizwa wala kulazimishwa, lila mmoja aende kwa hiyari yake bila vurugu.Msisitizo huo wa waziri kuhusu ulinzi, usalama, utulivu na amani ni vya muhimu kuzingatiwa na kila Mtanzania kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila viashiria vya uvunjifu wa amani.Kwa maana hiyo anawataka Watanzania kutumia haki yao ya msingi kwa kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo muhimu wa kuwapata viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji.Anahimiza hilo, kutokana na ukweli kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 8(1) (a); inayosema, wananchi ndio chimbuko la mamlaka ya utawala wa nchi na kwamba serikali itapata mamlaka toka kwao.Kwamba uchaguzi ndio njia pekee ya wananchi kukasimisha mamlaka yao kwa viongozi, na ni haki ya kila raia kushiriki katika michakato ya uchaguzi ikiwamo kupiga au kupigiwa kura kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Lengo kuu hapa ni kupata viongozi, hivyo ni muhimu serikali kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kushiriki katika chaguzi huo wa Serikali za Mitaa, na ninadhani ndiyo maana Waziri Mkuu akawahakikishia usalama.

Kwa hiyo, pamoja na sintofahamu iliyojitokeza ya vyama vya upinzani kususia uchaguzi huo, bado wananchi wanatakiwa kwenda kupiga kura kuchagua viongozi bila kuzuiwa wala kulazimishwa.Dhana ya haki ya kushiriki katika uchaguzi au uongozi ni muhimu, kwani ni  haki ya wananchi kushiriki katika masuala yanayohusu uongozi katika nchi yao kwa ajili ya maendeleo.

Habari Kubwa