Mpango aomba ufadhili njia nne Moro- Dodoma

20Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mpango aomba ufadhili njia nne Moro- Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika kuipatia Tanzania mkopo nafuu kwa ajili ya kujenga barabara ya njia nne kuanzia Morogoro hadi Dodoma ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.

Dk. Mpango alitoa ombi hilo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) anayewakilisha nchi nane za ukanda wa Afrika Mashariki, Amos Cheptoo.

"Barabara hii ilijengwa muda mrefu miaka ya 1980, malori mengi yanapita hapa kwenda Mwanza, Kigoma na nje ya nchi hasa Burundi na Rwanda na unaona kabisa imeelemewa na imeanza kuharibika, alisema.

Kutokana na hali hiyo, alimwomba Mkurugenzi Mtendaji waanze kuliweka jambo hilo kwenye miradi itakayogharimiwa na benki hiyo baadaye ili barabara hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuelekeza magari mawili kwenda upande mmoja na mengine mawili upande mwingine ijengwe.

"Baada ya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, tunahitaji usafirishaji kwa njia ya barabara uwe na tija zaidi, uende haraka zaidi lakini pia kupunguza ajali. Hivi sasa kuna ajali nyingi kwa sababu magari yanayokwenda Dar es Salaam na yanayokuja Dodoma au kwenda Mwanza yanapishana kwenye haka kanjia kamoja," alisisitiza.

Cheptoo aliyeko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, alisema benki yake itahakikisha Tanzania inapata mikopo ya miradi yake ya kimkakati na ya kipaumbele ukiwamo huo wa barabara ya Morogoro hadi Dodoma.

Katika hatua nyingine, Cheptoo ameitaka sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa za mikopo nafuu zilizoko katika benki hiyo.

Alisema sekta binafsi nchini ina nafasi nzuri ya kupata mikopo na utaalam utakaoiwezesha kujikwamua kiuchumi kwa lengo la kutokomeza umasikini katika Bara la Afrika.

"Sekta Binafsi hapa Tanzania haijatumia vizuri dirisha la mikopo ya sekta hiyo ikilinganishwa na nchi zingine za ukanda huu wa Afrika na ninakuomba Waziri wa Fedha na Mipango uihamasishe ikope fedha hizo ili kukuza mitaji yao na kuongeza tija," alisema Bw. Cheptoo

Aidha, alisema AfDB iko katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato Dodoma na tayari imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko mjini Dodoma na miradi mipya ya kuzalisha umeme ambayo iko mbioni kuwasilishwa katika vikao vya bodi ya benki hiyo hivi karibuni.

Habari Kubwa