Magufuli apokea ujumbe maalum wa Ramaphosa

20Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Magufuli apokea ujumbe maalum wa Ramaphosa

RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa matukio ya mashambulizi dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini sio msimamo wa Serikali ya nchi hiyo, na kwamba Serikali hiyo itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa kindugu na kihistoria na Tanzania.

Rais John Magufuli akipokea barua yenye ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, iliyowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum wa Rais huyo, Waziri wa zamani wa Nishati wa nchi hiyo, Jeffrey Radebe, baada ya kuwasili Ikulu jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Rais Ramaphosa alimtuma Mjumbe Maalum, Jeffrey Radebe, ambaye ni Waziri wa Nchi mstaafu wa Afrika Kusini aliyeongozana na Mshauri wa Rais wa Afrika Kusini katika masuala ya ushirikiano wa kimataifa, Dk. Khulu Mbhatha, kuwasilisha barua yenye ujumbe huo kwa Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam jana.

Katika ujumbe huo, Rais Ramaphosa alifafanua kuwa Afrika Kusini inatambua mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi na kupigania uhuru ambapo Tanzania ilijitolea kambi na misaada mbalimbali kwa wapigania uhuru.

Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli alisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Afrika Kusini, na kusisitiza ushirikiano zaidi katika maeneo ya biashara na uwekezaji.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alikutana na Mjumbe Maalum wa Waziri Mkuu wa Ethiopia ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Hirut Zemene Kassa.

Katika ujumbe huo, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, alimhakikishia Rais Magufuli kuwa Ethiopia itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Tanzania.

Rais Magufuli alisema Tanzania itadumisha na kukuza zaidi uhusiano wake na Ethiopia katika maeneo mbalimbali ikiwamo ushirikiano katika usafiri wa anga.

Habari Kubwa