Kupaa bei mahindi kwaishtua serikali

20Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Kupaa bei mahindi kwaishtua serikali

SERIKALI imekiri kupaa kwa bei ya mahindi kufikia Sh.107,000 kwa gunia huku ikiwataka watafiti  kufanyia kazi suala hilo  na kutoa mapendekezo ili kukabiliana na hali hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Siza Tumbo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Prof. Siza Tumbo, alisema hayo jana alipokuwa akifungua kikao cha uwasilishaji wa taarifa mbili za utafiti kuhusu kuimarisha usalama wa chakula na biashara ya mazao  ndani na nje ya nchi uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ESRF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Afrika (AGRA) na Wizara ya Kilimo.

Alisema utafiti huo ulitokana na kilio kilichokuwapo mwaka jana cha kuzuia uuzaji wa mazao ya chakula hususan mahindi nje ya nchi na kwamba mahindi yanatumika zaidi kwenye nchi za Afrika Mashariki.

"Kitu mnachotakiwa kuangalia kwenye kikao hiki ni bei ya mahindi ambayo imepanda sana kwa sasa. Watu wa mijini wameanza kuzungumzia hili, bei imeshafika Sh. 107,000 kwa mujibu wa takwimu zetu rasmi sasa kulinganisha na mwaka jana bei ilikuwa Sh. 65,000," alisema.

"Bei kwa sasa imepanda hatujui kwa sababu ya nini kwa sababu bei ya juu sana inafikiwa Februari kwa hiyo Februari, mwakani hatuna uhakika bei itakuwa sehemu gani. Kwa hiyo warsha hii pamoja na mambo mengine, ijadili hayo na kutoa mapendekezo namna ya kukabiliana na hali hii," alisisitiza.

Taarifa kutoka kwa waandishi wa mikoa mbalimbali jana zilionyesha kuwa bei ya gunia la mahindi kwa Ruvuma ni Sh. 65,000, Arusha (Sh. 97,000), Kilimanjaro (Sh. 107,000) na Iringa (Sh. 87,000).

Prof. Tumbo alisema kupanda kwa bei hiyo hakutokani na kukosekana kwa chakula, na kusisitiza kuwa chakula kipo.

"Tunaamini mtatoa ushauri mahsusi kwa Wizara ya Kilimo na tutauchukua namna gani twende mbele, hatuwezi kukwepa mahindi kwa kuwa ni zao linalopendwa sana na ni moja ya viashiria vya usalama wa chakula, bado tumefungua mipaka vyakula vinaenda nje na kuingia ndani,"alisema.

Aliwataka watafiti kutengeneza mfumo ambao utatumika kutoa muongozo kitu gani kinatakiwa kufanyika kwa wakati gani.

TANZANIA UCHUMI WA KATI

Katika hatua nyingine, alisema taarifa rasmi ya Benki ya Dunia inaonyesha kuwa Tanzania imeshafikia uchumi wa kati.

"Sasa hivi Tanzania tunachukuliwa kama hatujafikia uchumi wa kati, naomba wataalam wetu mjue kwamba tumeshafikia uchumi wa kati sasa hayo maandishi kuwa tuna mpango wa kufikia uchumi wa kati naomba mbadili. Taarifa rasmi ya Benki ya Dunia imeshasema Tanzania ipo kwenye uchumi wa kati isipokuwa hatujajikita katikati ya uchumi wa kati ndiyo tofauti," alisema.

Alibainisha kuwa kuna wakati Tanzania iliingia uchumi wa kati lakini ikateleza na kwa sasa imerudi tena na kwamba uwezekano wa kuteleza ni mdogo.

Habari Kubwa