Mbowe alazwa hospitalini

20Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam.
Nipashe
Mbowe alazwa hospitalini

HATIMA ya kufutiwa dhamana au kuachiwa kwa wabunge wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa na wenzake watatu wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi, itajulikana leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Pia mahakama hiyo ilielezwa mshtakiwa wa kwanza ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hakuwapo mahakamani jana kutokana na ugonjwa na kwamba amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam.

Wabunge wengine wanaoshikiliwa katika mahabusu ya Segerea, jijini Dar es Salaam kwa kukiuka masharti ya dhamana na kushindwa kufika mahakamani ni wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Jana mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ilisikiliza hoja za pande zote mbili wakiwamo washtakiwa na Jamhuri kuhusu utetezi wa kufutwa dhamana yao kwa kushindwa kufika mahakamani.

Mapema, kabla ya kusikiliza hoja hizo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Joseph Pande, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Mawakili wa Serikali, Jaqline Nyantori na Salim Msemo, ulidai kuwa mshtakiwa wa kwanza, Mbowe hayupo lakini wengine wanane wapo mahakamani.

Mdhamini wa Mbowe Grayson Selestine alidai kuwa mshtakiwa ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu amelazwa Hospitali ya Aga khan tangu juzi.

Washtakiwa kwa nyakati tofauti waliwasilisha hoja zao wakiomba huruma ya mahakama dhamana zao zisifutwe.

Msigwa alidai kuwa Novemba 15, mwaka huu asubuhi akiwa pamoja na Heche kwenye gari moja, walipata ajali mkabala ya jengo la Dar free Market na kwamba kwa sababu anaiheshimu mahakama, alilazimika kuchukua usafiri wa haraka bodaboda lakini alipofika alichelewa na kesi ilikuwa imeshapigwa kalenda.

"Wadhamini wangu mmoja amesafiri na mwingine amekihama Chama cha Chadema kwa hiyo sina mawasiliano naye, naiomba mahakama isinifutie dhamana," alidai Msigwa.

Mdee akiwasikisha utetezi wake alidai kuwa siku hiyo hakuwa sawa kiafya kutokana na kuumwa na kichwa na kwamba alifika mahakamani lakini alichelewa kesi likuwa imeshaahirishwa.

Wadhamini wake Mdee, kwa nyakati tofauti walidai kuwa mshtakiwa ni mwaminifu na kwamba mahakama isimfutie dhamana.

Heche alidai kuwa ni, mkazi wa Tarime hana makazi jijini Dar es Salaam hivyo hajawahi kuidharau mahakama kuacha kufika kusikiliza kesi yake lakini siku ya tukio alipata ajali akiwa ameongozana na Msigwa ikasababisha wachelewe kufika mahakamani.

Alidai wadhamini wake wote wamesafiri na walishindwa kufika mahakamani kumtolea udhuru na kuiomba mahakama isimfutie dhamana.

Bulaya alidai kuwa Novemba 14, mwaka huu alipata msiba wa mama yake mdogo mkoani Singida, hata hivyo, alimfahamisha mdhamini wake kuhusu msiba huo na kwamba ilikuwa ni lazima ahudhurie mazishi.

Alidai kuwa hajawahi kuidharau mahakama wala maofisa wa pande zote mbili katika kesi hiyo na kuiomba isimfutie dhamana.

Wadhamini wake Bulaya, Martha Charles na Joel Mwakalebela, kwa nyakati tofauti walidai kuwa walishtukia kesi imesha ahirishwa na walifanya juhudi za kufika kwa hakimu kumueleza lakini walijibiwa kwamba uamuzi wa mahakama umeshatolewa.

Wakili wa Serikali, Msemo alidai kuwa upande wa Jamhuri unawasilisha maombi mahakamani wakiiomba kuwafutia dhamana washtakiwa wanne kwa kukiuka masharti ya dhamana.

Alidai kuwa hakuna taarifa yoyote kutoka kwa washtakiwa hao zilizotolewa mahakamani siku ya kesi na kwamba mahakama ipuuze na iwafutie dhamana.

Pia, pamoja na mambo mengine alidai hoja ya Msigwa kudai kuwa mdhamini mmoja amehama chama na hana mawasiliano naye inaonyesha kwamba ana mdhamini mmoja.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa siku ya kesi mahakama ilitoa fursa kwa wakili wa utetezi, Faraji Mangula, kuwaita wadhamini kujieleza kuhusu mahali walipo washtakiwa.

Hata hivyo, hakujitokeza mdhamini yeyote mpaka mahakama ikatoa amri ya kukamatwa washtakiwa.

Mapema Ijumaa ya wiki iliyopita mahakaka hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washtakiwa hao kwa kukiuka masharti ya dhamana pamoja na wadhamini wao kwenda kujieleza sababu ya kutotimiza wajibu wao kuwapeleka washtakiwa mahakamani.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukiuka masharti hayo kwa kushindwa kufika mahakamani hapo bila kutoa taarifa.

Katika kesi hiyo Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki kwa Watanzania dhidi ya serikali.

Habari Kubwa