Meya wa Chadema Arusha atimkia CCM

20Nov 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Meya wa Chadema Arusha atimkia CCM

MEYA wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro (Chadema), amejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya kuchoshwa na vitisho vya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kutokana na uamuzi wake huo, Lazaro amejiuzulu nafasi zake za udiwani, umeya wa Jiji la Arusha, Uenyekiti wa Mameya na Madiwani wote wa Chadema na ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humprey Polepole, Lazaro alifika ofisi ndogo za chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam akidai kushindwa kuvumilia wakati mgumu aliokuwa anapitia katika utendaji wake wa kazi.

Taarifa hiyo ya Polepole ilidai Lazaro alipokea barua za onyo mara kadhaa kutoka kwa uongozi wa Chadema, wakimtaka kutotoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali na kutompongeza hadharani Rais John Magufuli.

Polepole alidai katika taarifa yake hiyo kuwa vitisho vya mara kwa mara ndivyo vimesababisha kiongozi huyo kujivua nafasi zake hizo na kujiunga na CCM.

Polepole pia alidai Lazaro ameeleza kuchukizwa na uamuzi wa Chadema kujitoa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

“Ndugu Lazaro amesema sasa yuko tayari kuchapa kazi ya wananchi akiwa ndani ya CCM na kwamba yupo tayari kwa maelekezo ya kazi kutoka uongozi wa chama hicho,” Polepole alidai.

Alisema Lazaro atapokewa rasmi na wanachama wa CCM Mkoa wa Arusha katika tarehe ambayo itapangwa.

Habari Kubwa