Kili Queens dimbani ikiwaza nusu fainali

20Nov 2019
Shufaa Lyimo
Nipashe
Kili Queens dimbani ikiwaza nusu fainali

WAKATI leo akikiongoza kikosi chake dimbani kuwavaa ndugu zao wa Zanzibar (Zanzibar Queens) kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge Cup) kwa Wanawake, Kocha-

Mkuu wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Queens), Bakari Shime, amesema akili yake sasa ni mchezo wa nusu fainali.

Juzi, kikosi hicho cha Shime kiliisambaratisha Burundi kwa mabao 4-0 ikiwa ni baada ya kuichapa Sudan Kusini mabao 9-0 katika mechi ya ufunguzi.

Na leo Kilimanjaro Queens itashuka dimbani kuivaa Zanzibar Queens katika mchezo ambao ni kama wakukamilisha ratiba kwa timu zote mbili kutokana na kikosi hicho cha Shime kufuzu hatua ya nusu fainali wakati ndugu zao hao wa Zanzibar wakiwa wameshaaga mashindano hayo kutokana na kupoteza michezo yote miwili.

Akizungumza na Nipashe jana, Shime alisema wamejipanga vizuri wakiwa na lengo la kuweka historia ya ubingwa kwa kutwaa kombe hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

"Nashukuru wachezaji wangu wamejituma mpaka tumefanikiwa kuingia hatua ya kucheza nusu fainali, kikubwa ni kuzidi kumtanguliza Mungu mbele," alisema Shime.

Alisema mashindano hayo yana ushindani na changamoto nyingi kutokana na timu zote kufanya maandalizi makubwa.

"Mashindano yana ushindani, kila timu imejipanga vizuri ili kupata ubingwa kila mchezo huwa tunacheza kwa tahadhari kubwa," alisema kocha huyo.

Aidha, alisema wamejipanga vizuri kukutana na Zanzibar Queens leo na lengo lao ni kuendelea kushinda hadi kulitwaa taji hilo.

Habari Kubwa