Kenya yatisha kwa hat-trick

20Nov 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Kenya yatisha kwa hat-trick

MICHUANO ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge Cup) kwa Wanawake, imeendelea kuweka rekodi ya kufungwa mabao mengi, lakini juzi rekodi mpya ikiandikwa kwa kupatikana penalti nne na hat-trick tatu katika mchezo mmoja.

Katika mchezo wa mapema jana, Djibouti iliendelea kuwa jamvi la wageni kwenye michuano hiyo baada ya kubugizwa mabao 12-0 dhidi ya Kenya kwenye mechi iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Hiki ni kipigo cha pili kwa timu hiyo, kwani kwenye mechi ya kwanza ilikumbana na dhahama ya kupigwa mabao 13-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda kwenye uwanja huo huo.

Kwa matokeo hayo, Kenya inasonga mbele kwa kutinga hatua ya nusu fainali kwenye Kundi B, baada ya mechi ya kwanza kuichapa Ethiopita mabao 2-0, hivyo kukusanya pointi sita.

Kwenye mechi hiyo, Mwanalima Adam alifunga 'hat-trick' kwa mabao yake ya dakika ya 34, 87 na 89, huku Mercy Airo akifunga naye 'ha-trick' kwa kutupia dakika ya 54 na 66 yote kwa penalti na akakamilisha dakika ya 61.

Mchezaji mwingine aliyefunga 'hat-trick' ni Jentrix Milimu dakika ya 16 kwa penalti kisha akarudi kambani dakika ya 14 na 56 kabla ya kutupia la nne kwa mkwaju wa penalti dakika ya 86. Janeth Bundi alifunga dakika ya 45 na Vivian Corazine alipachika bao lake dakika ya 15.

Habari Kubwa