Kaseja aiona Taifa Stars Afcon 2021

20Nov 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kaseja aiona Taifa Stars Afcon 2021
  • ***Asema sasa ni mwendo wa kupambana mwanzo mwisho, na kila mchezaji katika kikosi cha Ndayiragije ana...

KIPA chaguo la kwanza wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, amesema watapambana kwa nguvu zote hadi mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kwa lengo la kuhakikisha wanakata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2021.

Taifa Stars iliyoko chini ya kocha Etienne Ndayiragije, jana usiku ilishuka dimbani nchini Tunisia kuikabili Libya katika mchezo wa pili wa Kundi J wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakachezwa nchini Cameroon.

Akizungumza na gazeti hili kabla ya kuingia uwanjani jana, Kaseja, alisema wachezaji wa timu hiyo wanataka kuona Taifa Stars inashiriki kwa mara ya pili mfululizo kwenye fainali hizo kubwa, kwa sababu wanahitaji kuendeleza rekodi safi kwa timu hiyo.

Kaseja alisema wachezaji wengi walioko katika kikosi hicho wana ndoto za kucheza fainali hizo za Afcon na ili wapate nafasi ya kushiriki, wanatakiwa kupambana na wanaamini inawezekana.

"Tutapambana hadi mwisho, tunajua si kazi nyepesi, lakini kwa pamoja hakuna kitakachoshindikana, tunajiandaa na kujiweka tayari," alisema Kaseja, kipa huyo wa zamani wa Moro United, Simba, Yanga, Kagera Sugar na KMC FC, zote za hapa nchini.

Kaseja aliongeza kuwa kila mechi kwao ni sawa na fainali, hivyo hawatadharau mpinzani yeyote wanayekutana naye.

"Mechi zote tutacheza kwa nguvu na kasi inayofanana, tunajua wapinzani wetu pia wanajipanga kupata matokeo mazuri kila tutakapokutana nao, tunamuomba Mungu atuongoze kupata pointi iwe nyumbani au ugenini," Kaseja alisema.

Alisema pia anaendelea kumshukuru Ndayiragije kwa kumwamini na kumpa nafasi katika kikosi chake ambacho tayari kimeshapata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa ndani (CHAN), zitakazofanyika Aprili mwakani nchini Cameroon.

Kaseja ambaye alikuwa nje ya kikosi cha Taifa Stars kwa miaka sita, amechukua namba ya Aishi Manula wa Simba ambaye alikaa langoni katika mechi zote za kusaka tiketi ya kushiriki fainali zilizopita za Afcon na michezo mwili dhidi ya Senegal na Kenya huku Metacha Mnata akidaka katika mchezo dhidi ya Algeria.

Katika mechi ya awali ya kuwania ya Kundi J kuwania kufuzu Afcon 2021, Stars ilitokea nyuma na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Equatorial Guinea iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo wa jana Libya iliikaribisha Stars nchini Tunisia kutokana na kuwapo kwa machafuko ya kisiasa nchini kwao, jambo ambalo Shirikisho la Soka Afrika (Caf), lilihofia usalama wa wachezaji na kuwataka wenyeji hao kuchagua uwanja watakaoutumia nje ya nchi.

Habari Kubwa