Simba SC yatoa masharti usajili

20Nov 2019
Nipashe
Simba SC yatoa masharti usajili

WAKATI wachezaji wawili wa Simba, Rashid Juma na Saidi Ndemla wakitakiwa kwa mkopo kuelekea kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili mwezi ujao Desemba 16, klabu hiyo imetoa masharti mazito kwa timu zinazohitaji nyota wao.

Klabu ya KMC ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam inamuwinda dogo Rashid wakati Singida United ipo mawindoni ikihitaji huduma ya Ndemla ili kujinusuru na wimbi la kushuka daraja.

Lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa, amesema klabu yao itaweka masharti ya kuhakikisha mchezaji wao analipwa na timu husika kwa kiwango kile kile anacholipwa Simba kwa timu zinazowahitaji kwa mkopo katika dirisha dogo.

Mazingisa amesema Simba haitoruhusu klabu itakayomsajili mchezaji wake kumlipa mshahara ambao ni tofauti na wanaomlipa klabuni hapo.

Kocha wa Singida United, Ramadhan Nsanzurwimo ameonyesha nia ya kumsajili Ndemla ili akaokoe jahazi ambalo linaelekea kuzama wakati huu wakibuzura mkia kwenye Ligi Kuu wakiwa na pointi nne baada ya kushuka dimbani mara 11.

Kwa upande wa KMC iliyopo nafasi ya 16 ikiwa na pointi nane baada ya kushuka dimbani mara nane, uongozi wa klabu hiyo umeelezwa kuhitaji kwa udi na uvumba huduma ya Rashid ambaye naye hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba kama ilivyo kwa Ndemla.

Habari Kubwa