Mkoa una uhaba nafaka tani 92,627

21Nov 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Mkoa una uhaba nafaka tani 92,627

WAKATI Serikali ikishtushwa kwa kupanda kwa bei ya mahindi kufikia Sh. 107,000 kwa gunia, Mkoa wa Kilimanjaro unakabiliwa na uhaba wa mazao ya nafaka tani 92,627 ili kukidhi mahitaji ya wananchi wanaokadiriwa kufikia 1,906,978.

Hayo yalibanishwa na Ofisa Kilimo Mkoa wa Kilimanjaro, Saimon Msoka, katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya mkoa, ambapo alisema mahitaji ya chakula kwa mkoa  makadirio ya mwaka ni tani 452,431 za mafaka na tani 45,243 za protini (mikunde).

Msoka alisema kutokana na msimu wa kilimo cha masika 2018/19 ambao ndio msimu mkubwa, unyeshaji wa mvua haukuwa mzuri kwani zilianza kunyesha baada ya kuchelewa sana mwanzoni mwa Mei tofauti na ilivyozoelekea huanza katikati ya Machi.

“Licha ya mvua hizi kuchelewa kunyesha, pia ziliwezesha mazao kuota na daadaye mwanzoni mwa Juni zilikatika wakati mazao yakiwa bado katika hatua ya ukuaji hali ambayo iliathiri uzalishaji na kusababisha mkoa kuwa na upungufu wa chakula katika kipindi cha 2019/20,” alisema Msoka.

Aliongeza kuwa mahitaji ya chakula kwa mwaka ni tani 452,431 za wanga ambapo walizalisha tani 359,804, huku mahitaji ya protini ni tani 45,243 ambapo zilizozalishwa ni tani 61,614 kukiwa na ziada ya tani 16,371 za protini.

Alisema mikakati waliyojiwekea ili kukabiliana na upungufu wa chakula ni pamoja na viongozi katika ngazi zote kukumbushwa kuendelea kusimamia agizo la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, la kuwataka kutotumia nafaka hususan mahindi kutengenezea pombe za kienyeji.

Mkakati mwingine ni wakulima kushauriwa kuhifadhi vizuri mazao waliyovuna kwa kutumia teknolojia mbalimbali ili kuhakikisha mazao hayo hayaharibiwi na wadudu yakiwa ghalani pamoja na wananchi wenye upungufu wa chakula kujinunulia chakula na kujiwekea akiba wakati bei bado  hazijapanda.

“Tumekuwa tukiwashauri wananchi wenye mifugo kuuza baadhi ya mifugo yao ili kujipatia fedha za kununua chakula pia wafanyabiashara wa mazao tunawahimiza kununua vyakula kutoka sehemu zenye ziada na kuuza kwenye sehemu zenye mahitaji hasa mijini,” alisema Msoka.

Alisema katika msimu wa kilimo 2019/20 mkoa umelenga kulima hekta 311,381 za mazao mbalimbali ambazo zitazalisha tani 1,360,930 za mazao mbalimbali ya chakula na biashara ambapo mahitaji ya pembejeo msimu huu ni mbegu za mahindi tani 2,135, mbegu za mpunga tani 450, mbegu ya mtama tani 29.

Mbegu nyingine ni alizeti tani 77 na mbolea tani 14,163.05 ambapo pembejeo hizo zitapatikana kwa mawakala wa pembejeo waliopo katika maeneo mbalimbali katika halmashauri zote.

Habari Kubwa