Waziri asikitishwa kasi makusanyo kodi ya ardhi

21Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
GAIRO
Nipashe
Waziri asikitishwa kasi makusanyo kodi ya ardhi

KASI ndogo ya ukusanyaji mapato ya kodi ya pango la ardhi katika wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, imemsononesha Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula na kuagiza halmashauri hiyo kuongeza kasi ili kufikia lengo.

Akiwa katika ziara yake ya siku moja wilayani hapa juzi, Dk. Mabula alielezwa na Ofisa Ardhi wa Halmashauri hiyo, Nicolaus Matsuva, kuwa halmashauri hiyo katika kipindi cha mwaka 2018/19 ilikusanya  Sh. milioni 12.3 na mwaka huu kufikia Novemba, imekusanya Sh. milioni 10 wakati lengo ni Sh. Milioni 55.

Kutokana na taarifa hiyo, Mabula alisema kiwango hicho ni kidogo na hakijafikia hata nusu ya makadirio, hivyo kuitaka halmashauri hiyo kupitia idara ya ardhi, kuongeza kasi ya makusanyo ya maduhuli.

“Msipokusanya kodi ya ardhi mjue mnamkwamisha Rais kutekeza miradi mikubwa kama vile mradi wa kufufua umeme wa Mwalimu Nyerere maarufu  kama Stieglers Gorge, hivyo ni lazima tuongeze kasi ya makusanyao,” alisema.

Dk. Mabula pia aliitaka halmashauri kuhakikisha kufikia Desemba, mwaka huu, inarejesha Sh. milioni 31 ilizopatiwa kama mkopo kwa ajili ya upimaji viwanja.

Hatua hiyo ilitokana na Mabula kuhoji kuhusiana na marejesho ya fedha za mkopo huo na kuelezwa na ofisa ardhi kuwa halmashauri hajarejesha kiasi chochote cha fedha za mkopo iliopatiwa kwa ajili ya upimaji viwanja na kuomba kuongezewa muda hadi Machi, mwakani.

''Toka Juni hadi leo (juzi) hamjarejesha wakati ulitakiwa kurejeshwa ndani ya miezi mitatu. Mkopo huu unazunguka kwa nini hamjarejesha hadi leo? Kazi mliyopewa hamjamaliza, naagiza hadi Desemba fedha hiyo iwe imerejeshwa,” alisema Dk. Mabula.

Pia alishangazwa na idara ya ardhi katika halmashauri ya Gairo kuingiza viwanja 155 kati ya 1,198 kwenye mfumo wa makusanyo ya kodi ya ardhi kwa njia ya kielektroniki jambo alilolieleza linaikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi sambamba na kushindwa kutoa ilani kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ingawa ilani  hizo ziliandaliwa tangu mwezi Machi 2019.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Sirieli Mchembe, alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto ya ujenzi holela na kubainisha kuwa hata urasimishaji katika wilaya hiyo ni tatizo ikiwamo sebule za baadhi ya nyumba kuelekezwa kwenye vyoo vya nyumba nyingine.

Hata hivyo, alimwahidi Naibu Waziri kuwa ofisi yake itayafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa ikiwamo uandaaji wa mpango kabambe katika wilaya hiyo kupangika kimji sambamba na kuwa na mji wa serikali utakaojumuisha taasisi zote za serikali zilizoko katika wilaya hiyo.

Habari Kubwa