Wakili akwamisha kesi vigogo Simba

21Nov 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Wakili akwamisha kesi vigogo Simba

KESI inayomkabili Rais wa zamani wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na wenzake akiwamo Makamu wake, Godfrey Nyange, maarufu kama Kaburu, imeshindwa kuanza kusikiliza ushahidi wa utetezi kwa madai kuwa  Wakili wa Serikali anayeendesha kesi hiyo amepata udhuru wa kikazi.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa  kusikilizwa ushahidi wa utetezi lakini akadai kuwa wakili anayeendesha kesi hiyo amepata udhuru, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kusikilizwa.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Simba alisema kesi hiyo itasikilizwa ushahidi wa utetezi  Desemba 5, mwaka huu.

Mapema, mahakama hiyo iliwaona washtakiwa hao hawana kesi ya kujibu dhidi ya makosa ya kutakatisha fedha.

Aidha, washitakiwa hao waliachiwa kwa dhamani baada ya kufutiwa mashtaka mawili ya kutakatisha fedha Dola za Marekani 300,000 kutokana na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha.

Katika kesi ya msingi, shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Katika shtaka la tatu, Aveva na Kaburu  wanadaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka iliyokuwa ikionyesha Simba inalipa mkopo wa Dola 300,000 kwa Aveva kitu ambacho si kweli.

Aidha, Katika shtaka la nne, Aveva anadaiwa katika benki ya CRDB kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa kiasi hicho cha fedha.

Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.

Katika shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia Dola 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.

Aveva, Kaburu na Zacharia Hans Poppe  wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola 40,577 huku wakijua kwamba si kweli

Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola 40,577

Shtaka la tisa, Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola 40,577.

Habari Kubwa