Aussems awekwa kando rasmi Simba

21Nov 2019
Somoe Ng'itu
Nipashe
Aussems awekwa kando rasmi Simba
  • *** Achungulia dili la kuinoa Polokwane ya Afrika Kusini, Kaduguda, Try Again waula kwa kuteuliwa kuwa...

HAYAWIHAYAWI sasa yamekuwa! Hii ni baada ya uongozi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, kumweka pembeni Kocha wake Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems katika mechi ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba imefikia uamuzi huo kutokana na kukerwa na tabia ya kocha huyo kuondoka nchini na kudaiwa kwenda kwao Ubelgiji kwa matatizo binafsi bila ruhusa ya mwajiri wake. Hata hivyo, imedaiwa kuwa wala hakwenda Ubelgiji bali alikuwa nchini Afrika Kusini.

Taarifa zilizopatikana jijini jana kutoka chanzo chetu ndani ya klabu ya Simba, zimeeleza kuwa mabosi wa juu wa klabu hiyo wamesema kwamba kitendo kilichofanywa na Aussems si sahihi na wanaona si busara kumpa nafasi ya kukiongoza kikosi chao kwenye mchezo huo wa ligi.

"Aussems alikwenda Afrika Kusini kufanya mazungumzo ya kujiunga na klabu ya Polokwane inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo baada ya kuieleza Simba atakuwa nje ya Tanzania kwa muda wa siku tatu kutokana na kuwa na matatizo binafsi," kilieleza chanzo chetu.

Kutokana na Aussems kusimamishwa, kikosi cha vinara hao wa ligi kitaongozwa na Kocha Msaidizi, Dennis Kitambi pamoja na kiungo mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Mussa Hassan "Mgosi".

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingisa, juzi alinukuliwa akieleza kuwa Aussems alimtumia ujumbe ukimwarifu kuwa amepatwa na dharura lakini hakuainisha kuwa ameelekea wapi.

Kaduguda aula

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo, umemtangaza rasmi, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mwina Kaduguda "Simba wa Yuda" kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo ya jijini Dar es Salaam.

Kaduguda ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa Shirikisho la nchini -TFF) na Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), ndiye mjumbe mwenye muda mrefu ukilinganisha na wajumbe wengine wa bodi hiyo.

Uteuzi wa Kaduguda umeanza rasmi juzi na hiyo imetokana na uamuzi wa aliyekuwa Mwenyekiti, Swedi Mkwabi, kutangaza kujiuzulu kutokana na kubanwa na majukumu yake binafsi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Masingiza, ilisema pia imemteua Kaimu Rais wa zamani, Salim Abdallah "Try Again" kuwa Makamu Mwenyekiti wa bodi ya klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini.

Masingiza alisema pia katika taarifa yake kuwa bodi hiyo itatangaza hivi karibuni, tarehe rasmi ya uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi hiyo ya Mkwabi.

"Uteuzi huu umefanyika kwa mujibu wa Ibara ya 50 ya Katiba ya Simba ya mwaka 2018, tunaamini kila mmoja atatekeleza majukumu yake kikamilifu," alisema Masingiza.

Taarifa za ndani kutoka Simba zinasema kuwa kabla uamuzi wa kumtangaza Kaduguda kupewa cheo hicho, vilifanyika vikao mbalimbali ili kuweka mambo sawa na kuimarisha umoja ndani ya wajumbe wote wa bodi hiyo.

Habari Kubwa