Mpango aitaka Nida kurahisisha utoaji wa vitambulisho vya taifa

22Nov 2019
Mary Geofrey
Nipashe
Mpango aitaka Nida kurahisisha utoaji wa vitambulisho vya taifa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kurahisisha utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za fedha nchini.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo, ikiwa ni siku moja tangu Rais John Magufuli, kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Arnord Kihaule, kwenda mkoani Morogoro kushughulikia changamoto za utolewaji wa vitambulisho hivyo baada ya kupokea malalamiko kwa wakazi wa mkoa huo juzi, akiwa njiani kuelekea jijini Dodoma kwa ziara ya kikazi ya siku tano.

Akifungua mkutano wa 19 wa taasisi za fedha nchini, ulioandaliwa na Benki Kuu kwa kushirikiana na Umoja wa Benki nchini jana jijini Dar es Salaam, alisema anatambua juhudi zinazofanywa na serikali na wadau mbalimbali kuboresha sekta ya fedha ikiwamo kujenga kanzi data za taarifa za wateja na utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.

"Natoa rai kwa mamlaka husika kuharakisha utoaji wa vitambulisho vya taifa kwa upande mmoja na benki kuhakikisha wanaboresha utoaji huduma za kifedha," alisema Dk. Mpango.

Pia, Dk. Mpango, aliutaka mkutano huo wa siku mbili kujadili na kutoa mapendekezo ya mkakati ya kushusha riba ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa gharama nafuu na hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi.

"Riba ya mikopo bado ipo juu kiasi kwamba watu wengi wanashindwa kukopa na baadhi ya waliokopa kushindwa kurejesha. Hivyo licha ya juhudi za kuboresha sekta hii, ningependa mkutano huu utoe mapendekezo ya mikakati ya kushusha riba," alisema Dk. Mpango.

Aliwataka pia kujadili na kubainisha mikakati mipya ya kupunguza na kudhibiti kiasi cha mikopo chechefu katika benki.

Kadhalika alisema, mikopo kwa sekta kilimo siyo ya kuridhisha kwa sababu imekuwa chini ya asilimia tano ya mikopo yote itolewayo na benki.

Alisema sekta ya kilimo ni muhimu katika kutoa malighafi kwa ajili ya viwanda, chanzo kikuu cha chakula na fursa za ajira kwa Watanzania wengi na sekta yenye uwezo wa kupunguza umaskini na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni kwa kasi kubwa.

"Ni matarajio yangu kuwa mjadala wenu utaangalia namna bora ya kuzifanya taasisi za fedha kuongeza mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kilimo cha mazao, ufugaji, uvuvi na biashara husika," alisema Dk. Mpango.

Vile vile, aliwataka kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya taasisi hizo zinavyoweza kuchangia katika upatikanaji wa fedha za kugharamia miradi ya kimkakati ya serikali na ya sekta binafsi nchini.

Awali, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Florens Luoga, alisema sekta ya fedha imekua kwa wastani wa asilimia 3.1 na inachangia katika ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia 2.6 kwa kipindi cha miaka mitano iliyoishia 2018.

Alisema taasisi hizo zimeenea maeneo mbalimbali nchini na kwamba kuna benki 61 na matawi 838 nchi nzima.

Prof. Luoga alisema pia akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuongezeka na kufika Dola za Marekani bilioni 5.4 mwezi Oktoba mwaka huu na kiasi ambacho kinatosheleza kuagiza bidhaa kutoka nje kwa zaidi ya miezi sita.

Habari Kubwa