Hukumu ya Malinzi sasa Des. 5

22Nov 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Hukumu ya Malinzi sasa Des. 5

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema itatoa hukumu dhidi ya Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, na wenzake watatu, Desemba, mwaka huu.

Malinzi na wenzake hao wanakabiliwa mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha Dola za Kimarekani 173,335.

Hukumu hiyo iliyopangwa kusomwa jana lakini Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi, alisema bado haijakamilika na kwamba itasomwa tarehe iliyopangwa.

Kesi hiyo imesikilizwa na Hakimu Mkazi Maira Kasonde lakini kwa sasa amehamishwa kituo cha kazi

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kusikiliza hukumu na upande wa Jamhuri ulikuwa tayari.

Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisema hukumu ya kesi hiyo itasomwa Desemba 5, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Mapema mahakamani hapo, upande wa Jamhuri uliita mashahidi 15 na vielelezo tisa kuthibitisha kesi hiyo na utetezi ulileta mashahidi wanne kupangua tuhuma hizo.

Mbali na  Malinzi, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wako rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha ambayo ni miongoni mwa mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku Rauya akiwa  nje kwa dhamana.

Habari Kubwa