Aliyekatwa mkono aamuriwa kulipwa

22Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyekatwa mkono aamuriwa kulipwa

SERIKALI imetakiwa kumlipa fidia, Mariam Staford (36) mwenye ualbino baada ya kukatwa mkono na watu wasiojulikana nyumbani kwake mkoani Kagera, Oktoba 17, 2008.

Mariam Stanford ambaye alikatwa mikono yake miwili na watu wasiojulikana akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu uamuzi wa Kamati ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu iliyotoa hukumu baada ya kutoridhishwa na hukumu za mahakama za hapa nchini. Katika uamuzi wake kamati hiyo iliitaka serikali impe fidia, igharamie matibabu yake pia itoe visaidizi vitakavyomfanya aweze kuishi kwa kujitegemea. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under the Same Sun, Berthasia Ladislaus. PICHA: SELEMANI MPOCHI

Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu (CRDP) Septemba 19, mwaka huu, baada ya Mariam kupeleka malalamiko.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Shirika la Under The Same Sun (UTSS), Berthasia Ladislaus, alisema Mariam alikuwa akiilalamikia Serikali ya Tanzania kutompa haki yake ya kimsingi ya ibara ya 5, 6, 8, 10, 14, 15(1), 16 na 17 za Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu ambako Tanzania ni nchi mwanachama wa mkataba huo tangu mwaka 2009.

Berthasia alisema waliohusika na tukio hilo walikamatwa na kufunguliwa mashtaka katika Mahakama Kuu kanda ya Kagera, hata hivyo waliachiwa huru kwa kutokuwa na ushahidi wa kujitosheleza.

Kufuatia kutoridhishwa na mwenendo huo, alisema Mariam aliamua kutafuta haki yake kwenye vyombo vya kimataifa na Juni 12, 2014 aliamua kupeleka malalamiko yake kwenye kamati hiyo.

"Baada ya shauri hili kupokolewa katika kamati, Serikali ya Tanzania ilipata fursa ya kutoa maelezo na kujieleza mbele ya kamati Juni 25, 2015, lakini ilikanusha uwapo wa uvunjifu wa vifungu hivyo na kueleza kuwa ulinzi wa watu wenye ualbino umeimarishwa," alisema.

Alifafanua kuwa baada ya kujitetea katika kamati, Mariam alipata fursa ya kuwasilisha maelezo kinzani dhidi ya serikali Agosti 25, 2016 na alitoa utetezi wake uliokuwa na maelezo tofauti na kinyume na maelezo hayo ya serikali ikiwa ni hoja binafsi.

Kwa nyakati tofauti, alisema kamati iliiomba Serikali ya Tanzania kuwasilisha maelezo kinzani dhidi ya maelezo ya mlalamikaji, na ilipofika Januari 16, 2018 serikali ilikiri kupokea maelezo ya mlalamikaji, hata hivyo, haikuwahi kuwasilisha maelezo mengine ya ziada katika kamati hiyo hadi hukumu inatolewa.

"Kamati iliamua Serikali ya Tanzania impe fidia Mariam, igharamie matibabu yake, itoe visaidizi vitakavyomsaidia kuishi kwa kujitegemea, kufanya uchunguzi na upelelezi wa kina ili kuhakikisha wahalifu wote waliomdhuru Mariam wanasakwa na kuchukuliwa hatua," alisema Mkurugenzi huyo wa UTSS.

Alisema kamati imeiagiza Serikali ya Tanzania kufanya marejeo ya mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kuhakikisha haki za watu wenye ualbino zinalindwa ikiwamo usafirishaji wa viungo vya binadamu.

Lingine ni kuhakikisha kesi zote zilizoko mahakamani zinaisha na wahusika wanachukuliwa hatua, kuandaa programu za uelimishaji umma kuhusu hali ya ualbino.

"Kwa mujibu wa ibara ya 5 ya itifati ya mkataba huo, kanuni ya 75 ya kanuni za uendeshaji wa kamati, serikali inatakiwa kuwasilisha maelezo kwa kamati ndani ya miezi sita kuanzia Oktoba 15, mwaka huu juu ya hatua ilizozichukua kuhusu hukumu hii," alisema.

Hata hivyo, Mwanasheria wa UTSS, Maduhu Willium alisema hakuna kiasi maalum kinachopaswa kutolewa katika fidia, inapaswa kuendana na uhalisia wa madhara wa tukio.

Akizungumzia hukumu hiyo, Mariam alisema: "Nimefurahi kwa ushindi huu, ninachotaka ni utekelezaji wa maamuzi hayo".

Habari Kubwa