Mahakama yaamuru Lissu kufika mahakamani Des.19

22Nov 2019
Hellen Mwango
Nipashe
Mahakama yaamuru Lissu kufika mahakamani Des.19

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemwagiza mdhamini Ibrahim Ahmed wa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu Lissu-

-anayekabiliwa na kesi ya uchochezi kumtaka afike mahakamani Desemba 19, mwaka huu kusikiliza kesi yake.

Mahakama hiyo imesema kwa kuwa mdhamini ameieleza mahakama kwamba Lissu amepona, afike mahakamani siku iliyotajwa ili kesi iweze kuendelea.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya kumhoji mdhamini.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya hakimu na mdhamini:

Hakimu: Mdhamini wa mshtakiwa, Lissu yuko wapi?

Mdhamini: Mheshimiwa hakimu Lissu amepona, lakini amekataa kuja kwa sababu anahofia usalama wake.

Hakimu: Hatutaki mambo ya siasa hapa namtaka Lissu aje hapa mahakamani kesi yake iendelee.

Alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 19, mwaka na Lissu anatakiwa afike mahakamani siku hiyo.

Mapema mahakama hiyo iliagiza wadhamini wa Lissu kupeleka taarifa jana kuhusu mshtakiwa huyo.

Mbali na Lissu washtakiwa wengine ni, wahariri Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, 'Machafuko yaja Zanzibar.'

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Habari Kubwa