JPM awapa neno vibaraka ubeberu

22Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
JPM awapa neno vibaraka ubeberu

RAIS John Magufuli ametunukiwa shahada ya heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), na kubainisha kuwa miaka minne ya urais wake imemuimarisha na hakatishwa tamaa na vikwazo vya watu wanaotumiwa na mabeberu.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana katika mahafali ya 10 ya chuo hicho kilichomtunuku shahada hiyo kutokana na mafanikio mbalimbali ya kimaendeleo yaliyopatikana nchini chini ya uongozi wake.

Alibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya urais wake, kimemuimarisha na mafanikio mengi zaidi yatapatikana kama Watanzania watajituma na kutanguliza uzalendo mbele kwa kuwa Tanzania si nchi maskini.

"Si watu wengi ambao waliamini kuwa Watanzania wataweza kufanya mambo yote kwa kipindi kifupi, lakini tumeweza kwa kuwa mara zote Watanzania tukiamua hakuna linalotushinda.

"Miaka minne ya urais imeniimarisha, tukishikamana na kukusanya mapato, kuwa wazalendo, tutafanya makubwa zaidi," alisema.

Alieleza kuwa wapo wanaobeza na kukejeli, lakini nchi ni tajiri kutokana na kubarikiwa kuwa na rasilimali nyingi.

Alisema pamoja na kuwapo kwa mafanikio mbalimbali, vikwazo havikosekani na vingine vinaendelea kujitokeza.

"Kikwazo kimoja wapo ni jitihada zinazofanywa na mabeberu na vibaraka wao kwa kuwatumia wa ndani ya nchi kwa kujaribu kuweka vikwazo ili malengo yasitimie.

"Ndiyo maana kila mara mtasikia hili mara lile, ninyi ni mashahidi, sitaki kutaja yote mnayosikia, mara kuna mgonjwa huyu, mara kuna hiki, ni jitihada za kunifanya nikate tamaa, mimi sitakata tamaa.

"Miaka minne ya urais wangu nimejifunza uwezekano wa kuvishinda vikwazo hivyo upo na ni mkubwa sana ikiwa sisi Watanzania tutashirikiana na kushikamana kwa kutanguliza uzalendo na maslahi ya taifa mbele," alisema.

Rais Magufuli alieleza kuwa alipopata barua kutoka kwa Mkuu wa Udom, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, kuhusu kutunukiwa shahada hiyo, alijiuliza maswali mengi.

"Nilijiuliza maswali mengi sana na maswali haya sikupata majibu yake haraka: Kwanza, ilikuwa kwanini mimi; kwanini sasa wakati nimekuwapo siku zote? Lakini, swali lingine kwanini bila kusota?

"Inawezekana mzee bure alishakufa zamani, lakini nimeandikiwa barua na Rais aliyekuwa wa kwanza kuniteua kuwa naibu waziri, nitafanyaje?

"Baada ya kupata barua, nilikaa mwezi mzima bila kujibu, baadaye wasaidizi wangu walinikumbusha 'bado hujajibu barua ya Mzee Mkapa', nikawaambia nitajibu na bado nikachelewa.

"Dhamira yangu ilikuwa inanisuta 'kwanini nipewe cha bure?' Ile dhana niliyoipata kutoka kwa baba yangu kila kitu lazima nikisotee, dhamira ilikuwa inanisuta. Hata hivyo, pamoja na hayo yote, baada ya kukumbuka historia yangu na Mzee Mkapa aliponitoa, nikaona nikubali.

"Kingine kilichonifanya nikubali kutunukiwa, nikakumbuka shahada hizi huwa hazitolewi kwa kumpa mtu binafsi bali kwa niaba ya wengine, na imetolewa kwa kutambua mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano.

"Natambua si yangu binafsi, bali ni ya Watanzania wote, hasa wenye kuchapa kazi kwa bidii na kulipa kodi, kila Mtanzania mwenye kufanya hayo afurahie shahada hii," alisema.

Rais Magufuli alikumbusha kuwa mwaka 2015 Watanzania walidai mabadiliko ambayo yanahitaji kuwa na fedha na hivyo kulazimika kuongeza ukusanyaji mapato ya kodi kutoka Sh. bilioni 850 kabla ya Novemba 2015 hadi wastani wa Sh.trilioni 1.2 kila mwezi.

Alisema shahada hiyo imempa nguvu yeye na wasaidizi wake ya kujituma zaidi kutokana na kutambua mafanikio yaliyopatikana.

Alisema serikali yake pia inahitajika kudhibiti matumizi ya fedha ikiwamo kudhibiti safari za nje, kuondoa watumishi hewa na wenye vyeti vya kughushi, mikopo hewa, wanafunzi hewa, pembejeo hewa, likizo hewa, safari hewa na kile alichotania kuwa ndoa hewa na mapenzi hewa.

Alieleza kuwa waliamua kuwa fedha zipelekwe maeneo ya maendeleo hususani miradi mbalimbali ili kuleta tija kwa nchi kwa kuongeza bajeti yake.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Gaudencia Kabaka, alisema wameanzisha kitengo kipya chuoni kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika kazi kwa taasisi mbalimbali na kupunguza gharama zisizo na tija.

Alisema wametoa shahada hiyo kwa viongozi watatu hadi sasa ambao ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Rashid Kawawa na Rais Magufuli.

Habari Kubwa