Samatta afurahia kumponda Stars

22Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Samatta afurahia kumponda Stars

WAKATI wadau na wachambuzi mbalimbali wa soka nchini wakiponda na kueleza kutofurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, mshambuliaji huyo amefurahia namna wanavyomkosoa huku akieleza kwake anachukulia kama changamoto ya kufanya vizuri.

Katika michezo miwili ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) nchini Cameroon 2021, Samatta aliyeichezea Taifa Stars, wakati ikishinda 2-1 Uwanja wa Taifa dhidi ya Equatorial Guinea na ule wa nchini Tunisi wakipokea kipigo kama hicho kutoka kwa Libya, hakuonyesha ubora wake kama ambavyo amekuwa akiichezea klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji, jambo ambalo wadau wa soka wamejiuliza maswali mengi.

Miongoni mwa wadau wa soka walionukuliwa wakitoa maoni yao ni pamoja na Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' ambaye amemtaka Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mrundi, Etienne Ndayiragije, kutoona aibu ya kumuanzisha benchi Samatta.

"Inabidi Ndayiragije asione aibu kumuanzisha Samatta benchi ili ausome vizuri mchezo, unaona kama mechi ya juzi alicheza lakini mechi ilikuwa imemkataa kabisa," alisema Julio.

Hata hivyo, wapo waliomtetea Samatta wakisema, anakabwa na mabeki kuanzia wawili hadi watatu, hivyo wachezaji wenzake wa Stars ndio wanaopaswa kutumia mwanya huo kufunga mabao.

"Kwanza tazama, Samatta anavyokabwa na wenzake kubaki huru, lakini pia nani anayemchezesha kama ambavyo anakuwa akichezeshwa na wenzake pale Genk? Pia tukumbuke kuna siku mchezo unamkataa mchezaji na si suala kwamba anaogopa kuumia," alisema Ally Majaliwa mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Samatta kupitia akaunti yake ya Twitter @Samagol77, aliandika: "Nimepata meseji na Comment [maoni] kutoka kwa watu kadhaa kuwa hawajaelewa kiwango nilichoonesha katika mechi za timu ya taifa, 'anyway' ukweli nimefurahi kuona watu wanasema ukweli sichukii binafsi, bali nachukulia kama chachu itakayonifanya nijitume zaidi ili niweze [kuwa] bora zaidi. HAINA KUFELI."

Habari Kubwa