Waziri awabana wasafirishaji gesi asilia athari za mazingira

22Nov 2019
Na Mwandishi Wetu
KILWA
Nipashe
Waziri awabana wasafirishaji gesi asilia athari za mazingira

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima, ameagiza kituo cha kupokea gesi asilia cha Songas eneo la Somanga, kuwasilisha mpango kazi wa usimamizi wa mazingira unaoonyesha madhara na hatua zinazochukuliwa pindi yanapotokea maafa.

Sima alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake wilayani Kilwa mkoani Lindi, kukagua kituo hicho ambacho hivi karibuni kilipata tatizo la kuvujisha bomba la gesi katika eneo hilo.

Katika ziara yake hiyo, Sima alifuatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc) Prof. Esnat Chagu na Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo, Dk. Samuel Gwamaka.

Alisema ni muhimu wananchi wa vijiji zaidi ya 60 vilivyopitiwa na mradi wa bomba la gesi asilia kupatiwa elimu sahihi kuhusu faida za mradi huo na madhara pindi yanapotokea matatizo kama lililotokea juzi.

Naibu waziri huyo aliongeza kuwa nchi imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi na hasa gesi asilia huku akiwataka wahusika kuhakikisha mikataba inayoingiwa na makandarasi ionyeshe ushiriki wa wananchi na utolewaji wa elimu kwao kuhusu madhara ya gesi inapolipuka.

“Tumekuja hapa tuone kama miradi hii inafuata Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 na hapa tunataka tuone kwenye eneo hili yakitokea madhara ni hatua gani zinachukuliwa, tunataka kuona taarifa kamili na tuangalie kwenye eneo letu la mazingira mnachukua hatua gani.

“Hebu turudi kuangalia mkataba huu, makubaliano gani tunawekeana, siyo valvu mpya imetoka maabara imekuja ikawekwa hapa halafu ikajivusha gesi, hapana! Lazima tuje na majibu sahihi.

"Natambua wizara husika imefanya kazi yao na sisi tunaoratibu shughuli za mzingira, lazima tufanye kazi yetu," Sima alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nemc, Prof. Chagu alisema ni muhimu kwa wataalamu kuhakikisha vifaa vinavyotumika vinakuwa na viwango vilivyoidhinishwa na mamlaka husika.

Prof. Chagu alisema matumizi ya vifaa vyenye viwango yatasaidia kuhakikisha matatizo kama la hivi karibuni la kuvuja kwa gesi, hatokei na kusababisha madhara kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, alisema tukio la hivi karibuni la kuvuja kwa gesi lingesababisha madhara makubwa kama hatua za haraka zisingechukuliwa kudhibiti cheche za moto ambazo zilikuwa zinatokea.

Ngubiaga alibainisha kuwa, siku ya tukio, wananchi wanaotumia Barabara ya Kilwa, hasa waliosafiri kwa mabasi ya kwenda au kutoka Mtwara na Songea, waliathirika kutokana na kushindwa kuendelea na safari.Alisema athari za kiuchumi pia zilionekana kutokana na kuzimwa kwa Kituo cha Umeme cha Kilwa kwa saa kadhaa kulikoathiri maeneo mengi ya mikoa ya Pwani, Lindi, Dar es Salaam na mingine inayotumia umeme wa mkondo huo.

Habari Kubwa