Kilimanjaro Queens inaweza, tujitokeze Chamazi kuishangilia

23Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Kilimanjaro Queens inaweza, tujitokeze Chamazi kuishangilia

TIMU ya Taifa ya Tanzania Bara ya Wanawake, Kilimanjaro Queens, itashuka dimbani leo kuivaa Uganda kwenye mechi ya nusu fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge Cup) kwa Wanawake inayofanyika katika Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Kilimanjaro Queens, imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zake zote za Kundi A, ambapo ilianza kwa kuichapa Sudan Kusini mabao 9-0 kisha ikatoa kipigo cha 4-0 dhidi ya Burundi kabla ya kuhitimisha kwa kuwatandika ndugu zao wa Tanzania Visiwani, Zanzibar Queens kwa mabao 7-0.

Hivyo, Kilimanjaro Queens itaivaa Uganda ikiwa haijapoteza mechi hata moja wala kuruhusu nyavu zao kutobolewa kwenye michuano hiyo, ambayo inawania kulitwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo.

Lakini inakutana na Uganda ambayo imetoka kupoteza mchezo wake wa mwisho kwa mabao 3-0 dhidi ya Kenya baada ya kushinda miwili ya mwanzo kwa kuichapa Djibouti 13-0 na Ethiopia 1-0, na kushika nafasi ya pili katika Kundi B, ambalo Wakenya waliibuka vinara.

Kuelekea mchezo huo wa leo, tayari Kocha wa Kilimanjaro Queens, Bakari Shime ameeleza makosa madogo madogo ambayo ameyabaini katika mechi zilizopita ameshayafanyia kazi na kilichobaki ni vijana wake kutekeleza kile alichowaelekeza kukifanya dimbani leo.

Aidha, kuongezeka kwa ari na morali ya ushindi kama ambavyo Shime alilieleza Nipashe juzi, kunaongeza matumaini zaidi kwa Watanzania kuona Kilimanjaro Queens ikishinda mchezo wa leo na kutinga fainali kabla ya kuubeba kabisa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Tunaamini kwa kiwango kilichoonyeshwa na Kilimanjaro Queens katika michuano hiyo hadi kufikia sasa, itaendelea kutembeza vipigo hadi fainali na kilichobaki ni Watanzania kuendelea kuiombea ili iweze kuitoa nchi kimasomaso.

Lengo letu ni kutaka kuona kombe hilo linabaki nchini na Kilimanjaro Queens ikiandika rekodi kwa kulibeba kwa mara ya tatu mfululizo bila kuruhusu nyavu zake kutobolewa msimu huu.

Lakini pia, Nipashe tunatamani kuona wachezaji wa Kilimanjaro Queens wakishirikiana kumlisha mipira winga mshambuliaji, Donisia Minja, anayeshika nafasi ya pili kwa upachikaji mabao kwenye michuano hiyo, ili aweze kuibuka na Kiatu cha Dhahabu kwa kuwa mfungaji bora.

Hadi sasa Donisia anashika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao matano sawa na Nalukenge Juliet wa Uganda, wakiwa bao moja nyuma ya kinara Jentrix Shikangwa wa Kenya.

Hivyo, tunatamani kuona juhudi za dhati za ushindi kwa wachezaji wa Kilimanjaro Queens zikienda sambamba na kutoa pasi nyingi za mwisho kwa Donisia ili wakitetea ubingwa huo uende sambamba na Kiatu cha Dhahabu kubaki hapa nchini.

Hivyo, ili Kilimanjaro Queens na Donisia waweze kutekeleza hayo, ni wazi pamoja na kuiombea, lakini mchezaji wa 12 uwanjani ambaye ni mashabiki, ni muhimu sana katika kuwapa sapoti kwa kuwashangilia mwanzo mwisho.

Katika hilo, tunatamani kuona mashabiki na Watanzania kwa ujumla wakibadilika na kujenga utamaduni wa kushangilia mwanzo mwisho hata kama Kilimanjaro Queens itatangulia kufungwa.

Tunatambua Uganda itaingia uwanjani ikiwa na lengo la kupata bao la mapema ili kuweza kuunyamazisha uwanja, lakini hata kama ikitokea hivyo mashabiki hawana budi kuendelea kuishangilia Kilimanjaro Queens mwanzo mwisho ili kuwaongezea morali ya kufanya vizuri katika mchezo huo. Tunaitakia kila la kheri Kilimanjaro Queens.

Habari Kubwa