Bahati ina miujiza lakini haina ahadi

23Nov 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Bahati ina miujiza lakini haina ahadi

KWA kawaida bahati huweza kuleta mambo ya ajabu lakini haitabiriki. Kwa hiyo ni vigumu kuitabiri bahati. Methali hii yatuhimiza tufanye bidii bila kutegemea miujiza.

Timu mbili zinapopambana, kila moja huwa na lengo la ushindi, hasa moja inapocheza nyumbani. Timu ya nyumbani inaposhindwa na timu ngeni, washangiliaji wenyeji hunyamazishwa kabisa na wageni!

Husemwa “Bahati ni chudi” yaani bidii au jitihadi/tijihada. Methali hii yatufunza umuhimu wa kuwa na bidii katika mambo tufanyayo.

Kila timu inayoingia uwanjani kushindana na nyingine huwa na lengo la ushindi. Nathubutu kusema hata wendawazimu hawawezi kucheza ili washindwe! Ushindi ni hali ya mtu/watu kufanikiwa katika jambo alilokuwa/walilokuwa akiliwania/wakiliwania.

Wahenga walisema: “Mcheza kwao hutuzwa” wakiwa na maana kuwa mtu anayecheza kwao hupewa zawadi au kutunzwa vizuri. Methali hii hutumiwa kutufunza kwamba mtu anayelifanya jambo fulani vizuri au inavyopasa, hutuzwa au hupewa zawadi.

Mechi yetu ya kandanda dhidi ya Libya iliyochezwa Tunisia kisha Taifa Stars kupoteza kwa kufungwa 2-1 imekuwa na maneno mengi ya lawama dhidi ya wachezaji, hasa kapteni wao, Mbwana Samatta na kocha wao, Mrundi Etienne Ndayiragije.

Kwa waliofuatilia mchezo ule kwa makini watakubaliana nami kuwa Libya ilibebwa na mwamuzi (refa) wa mchezo ule kwa kuizawadia timu hiyo penalti ya bure.

Naandika hivyo kwa sababu chanzo cha penalti iliyopewa Libya na mwamuzi kutoka Malawi haikuwa halali kwani mpira uligonga ugoko/muundi (mfupa wa mguu kuanzia kifundo hadi kwenye goti) wa beki Bakari Mwamnyeto wa Taifa Stars na si mkono kama alivyoamua mwamuzi!

Tukio lile lilioneshwa kwa kurudiwa mara kadhaa (-a kiasi maalum) ili kuthibitisha mpira haukugusa mkono wa mlinzi wa Taifa Stars ila uligusa ugoko wake tu.

Kinachonishangaza ni kwa nini viongozi wa TFF waliofuatana na Taifa Stars hawakulalamikia dhuluma (kitendo cha kumnyima mtu haki au stahiki yake; uonevu) ile; au hawakuona?

Kama hawakuona, walisinzia? Kama ndivyo, walikwenda Tunisia kufanya nini? Au walikubaliana na uamuzi wa refa Mmalawi aliyechezesha mechi ile?

Kadhia hiyo inaiweka Taifa Stars katika hali ngumu kwani itabidi ishinde michezo iliyosalia bila kupoteza hata mmoja. Mechi hizo ni kati yake na Tunisia jijini Tunis na kurudiana nayo jijini Dar es Salaam.

Je, haiwezekani penalti ile ni sababu kubwa iliyowakatisha tamaa wachezaji wa Stars kipindi cha pili hata kufungwa bao la pili lililoipa ‘ushindi’ wa chee (rahisi) timu ya Libya?

Jambo lingine linalonikera ni upangaji wa michezo ya Ligi Kuu inayoendelea humu nchini. Kwa nini TFF inashindwa kabisa kupanga ligi ili timu zote zicheze mechi bila kutofautiana kwa idadi kubwa ya michezo?

Nilihesabu mechi za ligi za wenzetu zilizochezwa na timu za Ulaya msimu huu wa ligi yao mpaka Novemba 20, 2019 na kupata matokeo yafuatayo:

England: Mpaka tarehe niliyoitaja, timu 20 za ligi hiyo zilikuwa zimecheza mechi 12 kila moja. Hispania: timu zote 20 zilikuwa zimecheza michezo 13 isipokuwa mbili tu ndizo zilizocheza michezo 12.

Ujerumani: Timu zote 18 zilikuwa zimecheza mechi 11 kila moja wakati timu 20 za Italia zikiwa zimecheza mechi 12 isipokuwa timu mbili ndizo zilizocheza mechi 11. Ufaransa nayo ina timu 20. Katika hizo, timu 18 zimecheza mechi 18 ilhali timu mbili tu ndizo zilizocheza mechi pungufu, yaani 12 kila moja.

Tarehe hiyo hiyo niliyoandika makala unayosoma sasa, ligi ya Tanzania yenye timu 20 zikuwa zimecheza kama ifuatavyo:

Yanga mechi 5, Azam FC mechi 7, Simba FC, Polisi Tanzania na Ndanda FC mechi 9 kila moja. Kagera Sugar, Lipuli FC, Tanzania Prisons, Namungo FC, JK Tanzania, Alliance FC, Coastal Union na Biashara United zikiwa zimecheza mechi 10 kila moja,

Timu zilizocheza mechi 11 kila moja ni Mtibwa Sugar, Ruvu Shooting, Mbao FC na Singida United inayozibeba timu 19.

Haimaanishi kuwa timu za wenzetu hazina michezo mingine ya kimataifa, hasha! (sivyo kabisa.) Zinashiriki sana mechi za kimataifa ila zina mpangilio mzuri usiovuruga ligi zao.

Kinachowashinda viongozi wa TFF kuwa na mpangilio mzuri ili timu zetu kucheza mechi zisizotofautina kama wenzetu ni kitu gani?

Nadhani ni vema atumwe kiongozi mmoja ughaibuni akajifunze upangaji wa michezo ya Ligi Kuu kama inavyokuwa kwao. Najua kila mmoja atataka kwenda huko ili kufuta tongotongo.

Vinginevyo aalikwe mtaalam kutoka nje aje kusaidia upangaji wa timu ili zisiachane sana na kutoa nafasi kwa timu zinazotumia hela kuhonga timu zingine. Hakuna ubishi kuwa timu kubwa hufanya hivyo pindi zinapokuwa katika hali mbaya!

Timu zinazoitwa ‘ndogo’ hukubali kurubuniwa kwa kuwa zikikataa na kushinda michezo iliyosalia, haziwezi kutwaa ubingwa wala kushuka daraja.

Waliosema “fedha fedheha” walikuwa sahihi kabisa kwani huweza kuleta mambo ya aibu baina ya wanadamu. Methali hii yaweza kutumiwa kutuonya kuhusu maovu yanayosababishwa na pesa.

Ushauri wangu mwingine kwa TFF unahusu viwanja vya michezo, hasa kandanda kwa kuwa ndio mchezo upendwao sana nchini na duniani kote.

Shirikisho hilo lianze kupiga “Ya mgambo ikilia kuna jambo” pamoja na kuziandikia barua timu na taasisi zenye viwanja vyao kuvifanyia matengenezo muhimu.

Ikishindikana, timu zisizokuwa na viwanja vizuri zilazimishwe kucheza mechi zao kwenye Uwanja wa Uhuru na Taifa jijini Dar es Salaam, au Azam Complex n.k.

Ukitaka zuri sharti udhurike.

Habari Kubwa