JMP aonya utapeli wa fidia ya fidia

23Nov 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
JMP aonya utapeli wa fidia ya fidia

RAIS John Magufuli amewaonya wananchi kutotumia fursa ya makao makuu Dodoma kuwa chanzo cha kufanya utapeli kwa kutengeneza madai ya uongo ili walipwe fidia.

Magufuli alilisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi, soko la kisasa, ujenzi wa nyumba za askari wa kikosi cha kutuliza ghasia(FFU) na ujenzi wa hospitali ya Uhuru iliyoko wilaya ya Chamwino.

Alisema Dodoma kuwa makao makuu kusifanywe kama chanzo cha kuitapeli serikali bali watu wadai maeneo yanayostahili.

Alibainisha kuwa kuna watu wanafikiri hatua hiyo ni sehemu ya kutengeneza fedha za bure za serikali.

"Wanajidanganya sana kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Vijiji Na. 5, ardhi ya mtu ikichukuliwa ni lazima alipwe fidia lakini ardhi ya mtu ikichukuliwa si asili yake hawezi kulipwa fidia kwa kuwa alivamia anatakiwa kuilipa fidia serikali," alisema.

Rais alisema nyumba zilizopo eneo la Kisasa jijini Dodoma ameshiriki kuzijenga na watu wote katika nyumba hizo 300 walilipwa fidia.

"Kuna baadhi ya viwanja vya serikali vilipotea kwa watu binafsi na wapo viongozi wa serikali walijibinafsisha viwanja ambavyo ni mali ya serikali, ukisikia leo mtu anajitokeza anasema anadai fidia kwenye nyumba za kisasa unamshangaa kwasababu mimi nafahamu tulilipa zote, na nyaraka zilisainiwa hadi kwa Mkuu wa Mkoa kwa wakati ule," alisema.

Magufuli alisema katika eneo la kituo cha mabasi, soko na nyumba za askari akijitokeza mtu kudai fidia lazima amshangae.

"Kwa sababu eneo hili lilikuwa mali ya serikali na lilikuwa eneo la polisi walikuwa wakifanya mazoezi ya bunduki zao, sasa yeye alikuwa anakaa humo na bunduki zinapigwa, wakati nyani nao walikimbia," alisema.

Rais Magufuli alisema isifike mahali kila eneo mtu anasema ni lake watambue kuwa serikali ilikuwapo.

"Wapo kweli wachache kule Chamwino wanadai waliokuwa wamebaki, lakini asilimia zaidi ya 90 wamelipwa fidia wamebaki wachache, kuwa na makao makuu Dodoma msichukulie kama chanzo au fursa ya kutapeli serikali hilo halitawezekana serikali ina njia zake za kufanya kazi.

"Utapeli ni kosa la jinai, watu wadai maeneo wanayostahili ndio maana hapa nimewaletea viongozi ambao ni makini, watumieni hawa kutatua matatizo yenu," alisema

Rais alitolea mfano kuwa kuna eneo jirani na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), lilitengwa eneo la kuzika viongozi na alikataa kuzikwa Dodoma na kila mmoja alikataa kuzikwa huko, hivyo serikali ikarudisha eneo hilo kwa wananchi.

"Nawaomba ndugu zangu wa Dodoma tunapopeleka madai kwa serikali tuyapime madai, wamejitokeza matapeli mnawachangia na fedha wanajifanya mimi ndo nitakuwa mwenyekiti wa kamati ya kudai wale ni matapeli wanakula fedha zenu.

"Hata Dar es Salaam walijitokeza wakati tunajenga barabara ya Ubungo hadi Kimara tumebomoa bila fidia wakajitokeza mahakamani tukashinda kesi. Mjiepushe na matapeli kujenga makao makuu na serikali kuhamia sio fursa ya watu kupata fedha bure bure, serikali haina fedha za bure bure," alisisitiza.

Alifafanua kuwa anafahamu kukiwa na mikutano yake watu wanajitokeza wanalia.

"Mtu anatoka nyumbani halii akifika hapa analia lia, kwanini usitoke nyumbani unalia hadi hapa, wala siwasikilizi, sidanganywi wala sidanganyiki, we utalia hapa ukienda nyumbani utanyamaza lazima Dodoma tuijenge hatuwezi kuchelewa kuijenga Dodoma kwa mikwamo  ya hovyo, tumekuja kuibadilisha Dodoma.

"Kuna miradi mingi imejengwa Dodoma mambo ni mengi, lazima Dodoma ijengwe nawaambia wana Dodoma siku moja mtakumbuka, kuhamia Dodoma kulikuwa kumeshindikana Nyerere kazungumza tangu mwaka 1973 mimi nilikuwa darasa la sita, miaka 40 imepita, kuamua kuhamia hapa kunahitaji moyo wa kigogo,"alisema

Aliwataka kutokwamisha mafanikio yaliyopatikana kwa kuwa watu watawashangaa, makao makuu yangeweza kupelekwa hata mkoa wa Singida kwa kuwa ndio katikati ya nchi.

Hata hivyo, alisema wale wenye madai ya halali yashughulikiwe wasidhulumiwe.Kuhusu mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa soko na kituo cha mabasi, alimtaka kukamilisha kwa muda uliopangwa.

Kadhalika, alisema katika kituo hicho cha mabasi kuna eneo la wamachinga, hawatatozwa fedha yeyote bali watatumia vitambulisho vya ujasirimali walivyopewa.

"Hawa wenye vitambulisho hakuna kuwadai hela, bahati nzuri tutakuwa nipo tutabanana hapa hapa nitakuwa nikipita pita," alisema.

Alisema miradi yote ikikamilika Dodoma itakuwa ya kisasa.

"Tutaunganisha kituo cha mabasi na stesheni ili mtu akishuka apitilize moja kwa moja hadi ndani ya stendi, na pia tutaunganisha na uwanja wa ndege utakaojengwa wa Msalato lakini tutaunganisha na mji wa serikali, ili kurahisisha usafiri," alisema.

Hata hivyo, aliwatoa hofu wakazi wa Dodoma kuhusu changamoto ya maji na kudai kuwa ipo mbioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa ambalo litahudumia watu wa jiji la Dodoma na maeneo jirani.

Habari Kubwa