Tuungane kuishangilia Kili Queens itupe ubingwa leo

25Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Tuungane kuishangilia Kili Queens itupe ubingwa leo

LEO michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Challenge Cup) kwa Wanawake inafikia ukingoni kwa kupigwa mechi ya fainali itakayozikutanisha timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Queens na majirani zao, Kenya.

Katika mechi hiyo itakayopigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam majira saa 10 jioni, itatanguliwa na ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Burundi na Uganda saa saba na nusu mchana.

Kilimanjaro Queens imetinga hatua hiyo baada ya kuongoza Kundi A, ambapo ilianza kwa kuichapa Sudan Kusini mabao 9-0 kisha ikatoa kipigo cha 4-0 dhidi ya Burundi kabla ya kuhitimisha kwa kuwatandika ndugu zao wa Tanzania Visiwani, Zanzibar Queens kwa mabao 7-0.

Na katika hatua ya nusu fainali ikatoa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Uganda iliyomaliza nafasi ya pili katika Kundi B lililoongozwa na Kenya ambayo iliitoa Burundi katika hatua hiyo kwa kuifunga mabao 5-0.

Kwa ujumla mechi hiyo ya fainali ni ngumu hasa kutokana na ubora wa timu zote hasa ikizingatiwa Kenya nayo imefanya vizuri kuanzia hatua ya makundi ambapo katika Kundi lake la B ilitoa kichapo cha mabao 12-0 dhidi ya Djibouti, ikaichapa Ethiopia 2-0 na kisha ikaitandika Uganda 3-0.

Hivyo ni timu mbili ambazo zinakutana katika fainali zikiwa hazikupoteza mchezo hata mmoja huku pia zikiwa hazijaruhusu nyavu zao kutobolewa ambapo kwa Kilimanjaro Queens imefunga jumla ya mabao 21-0 wakati Kenya ikitingisha nyavu mara 17-0 hadi zinafika fainali.

Kimahesabu Kenya si ya kubeza hata kidogo, na inaonekana kuimarika na kuwa bora hasa ukizingatia, mpinzani wa Kilimanjaro Queens katika hatua ya makundi, Burundi na yule wa hatua ya nusu fainali, Uganda, Kenya iliwafunga kwa idadi kubwa zaidi ya mabao ukilinganisha na waliyofungwa na timu hiyo ya Tanzania Bara.

Wakati hatua ya makundi Kilimanjaro Queens ikiifunga Burundi 4-0 na kisha nusu fainali ikaifunga Uganda bao 1-0, Kenya yenyewe katika hatua ya makundi iliwachapa Waganda hao mabao 3-0 kisha nusu fainali ikawafumua Warundi hao 5-0, hivyo inaonyesha ni kwa namna gani Wakenya walivyo bora.

Hata hivyo, Nipashe hatuna wasiwasi kabisa kuhusu ubora wa Kilimanjaro Queens chini ya kocha mtaalam Bakari Shime, kuelekea mchezo huo wa leo ambao kama ikishinda itatwaa taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo, wakati Kenya hii itakuwa mara yao ya kwanza kulibeba endapo itaibuka na ushindi.

Tunaamini Shime atakuwa ameielekeza vema safu yake ya ulinzi namna ya kuwa makini katika kumkaba mshambuliaji Jentrix Shikangwa ambaye anaongoza katika orodha ya wafungaji akiwa na mabao tisa hadi sasa kwenye michuano hiyo.

Na si mshambuliaji huyo pekee, bali winga Mwanalima Jereko anapaswa kutazamwa vema na mabeki wa Kilimanjaro Queens kwani amekuwa bora zaidi katika ufungaji pamoja na kumtengenezea mabao Shikangwa.

Kinachotakiwa zaidi kwa Kilimanjaro Queens, mbali ya ilivyofanya kwenye mechi zilizopita, inatakiwa kuongeza umakini zaidi lakini pia ikicheza kitimu mwanzo mwisho ili kuweza kuibuka na ushindi.

Tunachotamani kukiona kikitokea ni kama ilivyo matamanio ya Watanzania wote kwa ujumla, ni Kilimanjaro Queens kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo na kutokubali katu kupoteza ikiwa katika ardhi yake ya nyumbani.

Tunatambua ili hilo liwezekane, mchezaji wa 12 uwanjani [mashabiki] wa kuwapa wachezaji hamasa ili kuweza kuongeza morali ya ushindi, ni muhimu kuwapo uwanjani, na kwa kulitambua hilo hatuna budi kuwahimiza Watanzania kujitokeza katika Chamazi leo ili kuishangilia Kilimanjaro Queens mwanzo mwisho. Nipashe tunaitaki kila la kheri Kilimanjaro Queens kushindi leo.

Habari Kubwa