Samatta kuwamo tu Stars ni ushindi tosha

25Nov 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Samatta kuwamo tu Stars ni ushindi tosha

MBWANA Samatta kama angekuwa ni Mganda, Mkenya, Mzambia au hata raia ya Madagascar tu, basi angepewa heshima kubwa tofauti na baadhi ya mashabiki wa soka la Tanzania wanavyomchukulia.

Baadhi ya mashabiki wa soka nchini wamekuwa wakitokwa na povu, wakimshutumu straika huyo kuwa anapochezea timu yake ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars hajitumi tofauti na anavyocheza kwenye klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji.

Baada ya mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu AFCON 2021 nchini Cameroon dhidi ya Equtorial Guinea, Taifa Stars ikashinda mabao 2-1 ilianza minong'ono na kipigo cha mabao 2-1 ugenini dhidi ya Libya kilisababisha mashabiki hao kupaza sauti zao kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Samatta ndiye anayeangusha Stars kwa sababu anakosa sana mabao.

Hali ikawa mbaya kwenye mitandao ya kijamii na kumfanya Samatta mwenyewe kujibu meseji ya baadhi ya mashabiki wa soka wanaomshutumu.

Alijibu kiukomavu wa hali juu. Akiwaambia amesikia na atajirekebisha. Kwangu mimi nadhani wanaomshutumu Samatta wanauangalia mpira kijuujuu au kishabiki zaidi.

Wanachoangalia pale kutaka Stars ishinde, tena bao lenyewe afunge Samatta. Hawauangalii mpira kiufundi na umuhimu wake uwanjani.

Kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Ubelgiji tangu atoke kucheza mechi za kuzufu AFCON, Samatta hajafunga bao, timu yake ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Royal Excel Mouscron.

Ina maana walifunga wachezaji wengine. Hili ndilo soka. Asipofunga yeye mwingine afunge. Asipofunga David Molinga, Juma Balinya afunge kwa Yanga na kwa Simba asipofunga Meddie Kagere, Miraji Athumani na afunge.

Haiwezekani Simba ikikosa ushindi alaumiwe Kagere kwa nini hafungi, au Yanga isiposhinda basi lawama zote kwa Molinga, hii si sawa kwa sababu soka ni mchezo wa ushirikiano zaidi na si kama ngumi ambapo anakuwa mtu mmoja tu ulingoni akipigana na mwenzake.

Samatta anapokuwa uwanjani hasa kwenye timu ya taifa, anakuwa anachungwa zaidi na mabeki zaidi ya mmoja au wawili.

Makocha wa timu pinzani ni rahisi zaidi kumuwekea mikakati ya kumlinda Samatta kuliko Ditram Nchimbi au Simon Msuva kwa sababu anacheza ligi Ulaya ambayo ni rahisi zaidi kuiona.

Nchimbi na wenzake ndiyo wanakuwa kwenye wakati mzuri zaidi wa kusumbua na kufunga kuliko Samatta mwenyewe ambaye anamulikwa na 'kijiji' uwanjani.

Wakati Samatta anatembea na mabeki wawili au watatu uwanjani, ina maana kuna wenzake anaocheza nao Stars hawana watu wa kuwakaba wanabaki huru.

Hawa wanafanyaje kuisaidia timu wakati wakiwa huru tofauti na mwenzao ambaye mgongoni kuna watu wanaomlinda?

Hata ukitazama akiwa anacheza Genk, Samatta huwa haangahiki sana, badala yake analishwa kwa pasi murua za mpenyezo na krosi au kona zenye macho na yeye kazi yake ni kufunga tu.

Je, Stars tumeziona pasi, krosi au kona za aina hiyo? Haiwezekani kwa sababu Samatta ni staa, basi awe anahangaika uwanjani kwa kila kitu, achukua mpira yeye apige chenga yeye na kufunga.

Straika huyo naona anatatizwa zaidi na kutokuwapo kwa wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi tena lile la ushindani.

Ndiyo maana nikasema kama ingekuwa kwenye mataifa ambayo yenye wachezaji wengi wanacheza soka nje tena kwenye ligi za ushindani, au kuwa na wachezaji ambao wenye viwango vya juu na kujua jinsi ya kuchezesha, basi angekuwa anafanya vitu vikubwa zaidi ya hivi. Baadhi ya Wabongo wasijidanganye kutaka eti asipangwe kwenye mechi zinazofuata.

Kuwapo kwake uwanjani tu kunasababisha hata wapinzani wacheze kwa woga na wasipande wote na kuwa salama kwa Stars.

Na itakuwa ni vichekesho kwa mataifa mengine duniani kwa timu kama ya Tanzania ambayo haina wachezaji wa viwango vya juu kama yeye, kumuweka nje au kumuacha na kuchezesha wachezaji wengine.

Waswahili wana msemo 'kondoo hajui thamani ya mkia wake hadi ukatwe'. Chondechonde, tusiombee hali hiyo isije ikajitokeza Stars.

Habari Kubwa