Uchaguzi mitaa wananchi wanahitaji kuujua ukweli

27Nov 2019
Elizaberth Zaya
Nipashe
Uchaguzi mitaa wananchi wanahitaji kuujua ukweli

UCHAGUZI wa serikali za mitaa umemalizika huku Chama Cha Mapinduzi(CCM) kikishinda vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9.

Chama hicho pia  kimeshindia  katika mitaa 4,263 sawa na asilimia 100 katika matokeo ya jumla na katika nafasi ya mwenyekiti kimeshinda vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4, kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa (Tamesemi), Selemani Jafo, ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kusimamia uchaguzi.

Baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo vilikuwa vimetangaza kutokushiriki katika uchaguzi huo navyo vilipigiwa kura kikiwamo chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi(CUF) na ACT-Wazalendo.

Japokuwa vilitangaza kujiondoa lakini nembo za vyama vyao vilionekana katika karatasi za kupigia kura na hivyo wananchi wakatekeleza wajibu wao kwa kuwapa kura.

Vyama hivyo vilitangaza kujiweka pembeni katika uchaguzi huo kwa madai ya kutoridhishwa na mchakato mzima wa kukubalikwa kwa uteuzi wa wagombea wake, vikilalamika  kutokuteuliwa kwa wagombea wake bila kuwapo na sababu za msingi.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi na Waziri Jafo, vyama hivyo navyo vilipigiwa kura, ambapo  Chadema na CUF vilipata ushindi katika kijiji kimoja kimoja na katika nafasi ya wenyekiti ACT-Wazalendo nacho kilishinda kitongoji kimoja.

Jafo alisema jumla ya nafasi zilizogombaniwa ni 332,160 ambazo zote zilihusisha katika uchaguzi wa vijiji 12,262, mitaa 4,263, vitongoji 63,992, wajumbe kundi la wanawake 106,622 na wajumbe  kundi la mchanganyiko 145,021.

Katika nafasi ya wenyeviti, Chadema ilishinda nafasi moja  ya wenyeviti wa vitongoji(19), kundi la wanawake(39), wajumbe kundi la mchanganyiko (71), huku CUF nayo ikipata nafasi moja ya kijiji, vitongoji viwili, wajumbe kundi la wanawake nafasi tatu na wajumbe kundi la mchanganyiko nafasi 14.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, baadhi ya  vyama hivyo ambavyo vilikuwa vimetangaza kujitoa katika uchaguzi huo vilikuja juu kwa nembo yao kutumika katika uchaguzi.

Miongoni mwa vyama vilivyolalamika ni pamoja na CUF, Chadema, na ACT-Wazalendo.

Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya, anasema wanashangaa nembo ya chama chao kutumika katika uchaguzi huo wakati walijitoa na kwamba msimamo wa chama hicho bado uko pale pale  kwamba hawakushiriki  katika uchaguizi huo.

Chama cha ACT-Wazalendo nacho kupitia Katibu Mwenenzi, Ado Shaibu, kinasema msimamo wa chama hicho haujabadilika na kwamba walisikitishwa na nembo ya chama chao kutumika katika uchaguzi huo

Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, anasema wanakusanya vielelezo na watatoa ushahidi kwa halmashauri zote zilizokiuka agizo la chama hicho.

Kwa yote haya yaliyotokea katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa uliomalizika juzi, kuna jambo la kujifunza ili kuhakikisha kwamba katika uchaguzi ujao kusitokee tena kama yaliyojiri safari hii.

Funzo hilo linapaswa liwe kwa makundi mbalimbali ikiwamo kwa vyama vya siasa vyenyewe, mamlaka husika zinazohusika na masuala ya uchaguzi, viongozi wanaosimamia mchakato mzima wa uchaguzi huo.

Wahusika wajiulize kama kuna mahali wasimamizi au mamlaka na uchaguzi zilifanya makosa na kusababisha kutokea upungufu wajirekebishe, wakae chini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizojitokeza na kutoa maelezo kwa wananchi.

Kabla ya baadhi ya vyama hivyo kujitoa katika uchaguzi huo, yapo maandalizi ambayo wagombea wa vyama hivyo  walikuwa wamejipanga kabla ya kutangaziwa kwamba wasishiriki kutoka kwa viongozi wao wakuu.

Na kwa kuwa ilikuwa ni agizo au amri kutoka kwa viongozi wao, kwa kupenda au kutokupenda walikubali kutoshiriki, lakini je waliridhika na uamuzi huo?

Ni vema mambo haya yakatazamwa kwa undani na kuyatenda kwa haki bila kuathiri upande wowote au kuumiza mtu hasa katika uchaguzi mwingine unaokuja viongozi wawashirikishe wananchi wasiamue kufanya kila wanachoona kinawafurahisha.

Habari Kubwa