Mradi huu utawakomboa wahitimu wa elimu ufundi

27Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Mradi huu utawakomboa wahitimu wa elimu ufundi

KUNA taarifa njema zinazoeleza kuwa serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, wanatekeleza mradi wa kuleta mapinduzi kwenye elimu ya ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi, Dk. Leornad Akwilapo, alisema katika utekelezaji wa mpango huo, benki hiyo imetoa Dola za Marekani milioni 75 (Sh. bilioni 172.4) katika vyuo vinne ambavyo ni Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) kampasi ya Dar es Salaam na Mwanza pamoja na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Kwa mujibu wa Akwilapo, fedha hizo zinatolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya kuvijengea vyuo hivyo uwezo ili kutoa wanafunzi wenye ujuzi stahiki wa kuwawezesha kujiajiri ama kuajiriwa na pamoja na kuvijengea vitu vya umahiri.

Katibu Mkuu huyo, aliyemwakilisha Waziri wa wizara hiyo, Prof. Joyce Ndalichako, alisema mradi huo utawezesha kujenga miundombinu bora na kuweka vifaa pamoja na kuwajengea uwezo wakufunzi.

Aliwataka Watanzania kufahamu kuwa elimu ya ufundi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi hasa katika uchumi wa viwanda, na kwamba vyuo vya ufundi visiwe chaguo la mwisho kwa mtu anayefeli.

Kwamba fedha hizo zitatumika katika kuhakikisha wanawajengea uwezo wanafunzi na wanapohitimu inakuwa rahisi kuajiriwa viwandani na hasa ikizingatiwa Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda.

Mpango huo tunauona ni mzuri na utakuwa na manufaa kwa nchi yetu ambayo ajira kwa vijana imekuwa moja ya changamoto kubwa kutokana na serikali kutokuwa na uwezo wa kuajiri wahitimu wengi wanaotoka kwenye vyi vikuu na vya kati.

Hatua ya kuwezesha vyuo vya elimu ya ufundi bila shaka itajaribu kupunguza mahaki ya ajira, kwa sababu vyuo hivyo vitasaidia kuzalisha vijana ambao wakishahitimu hawatahangaika kutegemea kuajiriwa na serikali bali watajiongeza kwa kujiajiri wenyewe.

Ni wakati mwafaka sasa kwa vijana wetu wanaosoma elimu ya ufundi kwenye vyuo tajwa kuuchukulia mradi huu kama fursa adhimu ya kujiletea maendeleo.

Fursa nyingi zipo kwenye kozi wanazochukua kwa sababu kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi huo kutoka Wizara hiyo, Dk. Noel Mbonde, vyuo hivyo vinne vimejikita katika masuala ya Teknolojia ya Habari (Tehama), gesi asilia, ngozi na masuala ya anga.

Jambo la msingi ni kuwa wahusika; kwa maana ya watekelezaji wa mradi wahakikishe kuwa fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia zinatumika kwa mujibu wa malengo, na kwa kufanya hivyo kutawajengea imani ya kuendelea kusaidia.

Lakini pia serikali yetu iendelee kubuni na kutekeleza miradi mingine ya kuvipatia uwezo zaidi vyuo vya ufundi hususan na ufundi stadi vilivyoko chini ya Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) ili wahitimu wake wamudu ushindani katika soko la ajira na wakati huohuo kujiajiri wenyewe.

Ikumbukwe kwamba wakati huu ambao Tanzania imepania kuingia katika uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, viwanda vitakavyoanzishwa vitawahitaji wataalamu hao na wengine wanakuwa na fursa ya kuanzisha viwanda vyao vidogo.

Hatua ya msingi kwa wizara husika ni kubuni mikakati ya kuzalisha wahitimu bora katika vyuo vya ufundi ngazi zote, Pia serikali itenge fedha zaidi kwa ajili ya kuviwezesha vyuo hivyo.

Bila kufanya jitihada hizi, tunaweza kujikuta bila kuwa na hata mafundi mchundo kwenye viwanda vitakavyojengwa, hivyo kutegemea wa kutoka nje ya nchi.

Habari Kubwa