Idadi kubwa ya walimu waliofukuzwa inatisha

28Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Idadi kubwa ya walimu waliofukuzwa inatisha

TAARIFA kuwa walimu 4,046 wamefukuzwa kazi ndani ya miaka mitatu kwa utovu wa nidhanu ni za kusikitisha na kutisha, hivyo kuna umuhimu wa kulitafakari suala hili.

Ni jambo la kusikitisha kwa kuwa bado taifa letu lina mahitahi ya walimu kwa ajili ya kuwafundisha watoto wetu katika shule zilizotapakaa maeneo mengi ya nchi.

Hayo yalibainishwa juzi na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutaindurwa, na kufafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, idadi ya walimu waliofukuzwa kazi ni sawa na asilimia 70 ya waliopewa adhabu kutokana na makosa ya kinidhamu.

Aliyasema hayo juzi jijini Dodoma alipotoa taarifa ya tume kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuundwa kwake wakati wa kikao kazi cha kaimu makatibu wasaidizi wa wilaya nchini.

Alisema walimu 930, sawa na asilimia 16.2 ya waliopewa adhabu, walipewa onyo na wengine 284, sawa na asilimia 4.9, walipunguzwa mshahara. Vilevile, alisema walimu 244, sawa na asilimia 4.2 ya waliopewa adhabu, walisimamishiwa nyongeza ya mshahara.

Kwamba walimu wengine 237, sawa na asilimia nne ya waliopewa adhabu, walishushwa cheo na walimu 14, sawa na asilimia 0.2 ya waliopewa adhabu, walifidia hasara.

Rutaindurwa alisema makosa ya kinidhamu yaliyofanywa na walimu katika kipindi hicho cha miaka mitatu ni pamoja na utoro kazini (makosa 5,447, sawa na asilimia 76.5 ya makosa yote).

Makosa mengine ni kukiuka maadili (makosa 1,290 sawa na asiilimia 18.1, uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi 162 (asilimia 2.3). Makosa mengine kwa ujumla wake yalikuwa 224, sawa na asilimia 3.1 na vilevile katika kipindi cha miaka mitatu, adhabu zilizotolewa ni 5,753.

Taarifa ya Rutaindurwa kwamba asilimia 76.5 ya makosa yote ni utoro ni suala linalotisha ma kusikitisha. Aidha, hali hiyo inathibitisha madai ambayo yamekuwa yakitolewa mara kwa mara kuwa walimu wengi ni watoto kazini, hivyo hiyo ni changamoto kubwa ambayo inapaswa kufuatiliwa na kupatiwa ifumbuzi na mamlaka husika.

Tunasema hivyo kwa kuwa utoro wa walimu ni kosa kubwa ambalo linawaathiri sana wanafunzi moja kwa moja kitaaluma, kwa kutilia maanani kuwa kwa sasa serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi, ambayo ndiyo inayomiliki shule zote na walimu bila shaka imepewa taarifa hizi na tunaamini kuwa viongozi wake wakiongozwa na Waziri Selemani Jafo watafuatilia na kuchukua hatua.

Jambo la msingi ambalo serikali inapaswa kulitafutia majawabi ni kwa nini walimu wanakuwa watoto kazini wakati wanalipwa mishahara na serikali?

Kwa upande wetu Nipashe, tunaona kuwa sababu ya utoro wa walimu kazini ni kukosekana kwa taratibu za kuwafuatilia wawapo kazini. Miaka ya zamani idara ya ukaguzi ilipokuwa chini ya Wizara ya Elimu kulikuwapo na ufuatiliaji wa karibu wa walimu kutokana na ukaguzi wa mara kwa mara shuleni.

Hata hivyo, kwa sasa inaonekana ndani ya Tamisemi kuna udhaifu wa ukaguzi katika shule, hivyo, tunaishauri wizara kuangalia uwezekano wa ‘kuiamsha’ idara hiyo ikiwamo kuiwezesha kwa vifaa na fedha ili itekeleze vyema majukumu yake katika mazingira rafiki. Tunaamini kwa kufanya hivyo, itakuwa ni rahisi kupunguza utoro wa walimu kama siyo kuumaliza kabisa.

Habari Kubwa