TGNP- Mtandao inavyomtaka mwanamama kuchangamka

28Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
TGNP- Mtandao inavyomtaka mwanamama kuchangamka

HISTORIA inaonyesha mchakato wa kupigania haki za wanawake kote duniani, ulianza takriban karne moja iliyopita na bado juhudi za kupigania zinaendelea, ili kuhakikisha, kile kilichokusudiwa kinatimia.

Nchini kwetu, serikali na wadau mbalimbali zikiwamo asasi za kiraia kama TGNP Mtandao, wamekuwa mstari wa mbele kutetea haki za wanawake ili kuhakikisha wanashiriki kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo, bila kusahai mustakabali wa uchumi.

Lengo kuu ni kutaka kuwapo usawa kati ya mwanaume na mwanamke kwenye ngazi za maamuzi na hata kusimamia shughuli za maendeleo, ikiwamo umiliki wa viwanda vya kuzalisha mali, vidogo na hata vikubwa inapobidi.

Hapa ngoja nitaje baadhi ya haki zinazopiganiwa kwa ajili ya kumkomboa mwanamke, ambazo ni usawa kijinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii, kisiasa katika kufikia maendeleo jumuishi.

Nikiri nchini Tanzania, kuna jitihada mbalimbali zilizofanywa na jamii, serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kumwinua mwanamke.

Kwa upande wa asasi za kiraia, asasi hii ya TGNP Mtandao, ni miongoni mwa walio mstari wa mbele kupigania haki za mwanamke katika nyanja zote na hasa wakati huu, nchi inaelekea kuwa ya viwanda.

Hii inatokana na ukweli kwamba, haki na usawa katika hilo. ndiyo mambo makuu yanayoshinikizwa duniani kwa ajili ya kufanya mabadiliko, kuhimiza na kuwawezesha wanawake wa nyanja zote kutambua uwezo wao.

Licha ya kwamba mwanamke anachangia katika ukuaji uchumi, bado baadhi ya maeneo hayajashirikishwa kikamilifu, kwani mwanajinsia huyu amekuwa akikutana na vikwazo na anapata ajira zenye vipato vya chini na pia nafasi finyu ya kujiendeleza.

Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa, ili kutimiza, malengo ya maendeleo endelevu kama sehemu ya ajenda ya mwaka 2030, kuna haja ya kuisaidia Afrika kushinikiza ustawi endelevu wa kiviwanda na unaojumuisha kila mtu.

Baadhi ya nchi za Afrika ikiwamo Tanzania, zinapania kuwa na nchi zilizoendelea kiviwanda, lakini kwa mara nyingi idadi kubwa ya wanawake wanaonekana kususia kujitosa katika sekta hiyo.

Lakini, ni bahati nzuri serikali ya Tanzania ilisharidhia Itifaki ya Maendeleo na Jinsia ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), inayosisitiza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi kitaifa.

Katika taifa lililoridhia itifaki hiyo ya maendeleo, Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 37 ya wanawake bungeni, asilimia 41 wanawake majaji na asilimia 30 kinamama madiwani. Ni hatua nzuri, japo inahitaji kusonga zaidi.

Kutokana na jitihada hizo, wanawake wanaendelea kuaminika na kuchukua nafasi za juu za uongozi na maamuzi. Tunawashuhudia sasa wachapa kazi kama wakuu wa wilaya, wakurugenzi na vyeo kama hivyo.

Hivyo, wakati huu ambao nchi inaelekea kuwa ya viwanda, bado kuna uhakika kuwa wanawake hawataachwa nyuma, kutokana na ukweli kwamba uchumi unajengwa na Watanzania wa jinsia zote.

Pamoja na jitahada hizo za kuwezesha wanawake, siyo vibaya wadau wengine kama nilivyowataja TGNP Mtandao, wakaendelea kutia joto ili kuhakikisha wanawake hawabaki nyuma kwenye maendeleo ya nchi yao.

Ninaitambua Siku ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa kila Machi 8 ya mwaka, ikilenga kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali na kumuinua kimaendeleo.

Kuna maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyowahi kuwa na kaulimbiu isemayo: "Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini’.

Kwa maana hiyo, wawe wanawake wa mijini na vijijini, wote wanatakiwa kusaidiwa, kwa kila hali ili kuhakikisha wanakuwa na mchango katika Tanzania ya Viwanda.

Hata wanawake wakulima, wanatakiwa kupata elimu ya kukuza biashara zao na kuona thamani ya kile wanachokifanya kwa kuboresha huduma zao na kutengeneza mnyororo mpya wa thamani.

Kwa kufanya hivyo, ni wazi kwamba watakuwa na mchango mkubwa kwenye Tanzania ya Viwanda, kwani viwanda vinavyojengwa vimo ambavyo vinategemea mazao kutoka kwa wakulima, wakiwamo wanawake.

Hivyo, jitihada zinazofanywa na asasi za kiraia, ikiwamo TGNP Mtandao, kwa ajili ya kutambua mchango wa mwanamke hasa wakati huu wa kuelekea Tanzania ya Viwanda, hazina budi kuungwa mkono na wadau wote.

Hata urasimishaji wa vikoba na kuwashawishi wanawake wengi zaidi kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii, ili kuweza kunufaika na mafao na mikopo itolewayo na taasisi hizo, bado ni njia mojawapo ya kumwezesha mwanamke, hizo nazo ziungwe mkono.

Habari Kubwa