Miraji ajipanga kufanya makubwa Simba, Stars

28Nov 2019
Shufaa Lyimo
Nipashe
Miraji ajipanga kufanya makubwa Simba, Stars

MSHAMBULIAJI wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, Miraji Athumani "Sheva", ameahidi kuendelea kujituma zaidi ili kuisaidia klabu yake kutimiza malengo ya kutetea taji hilo wanalolishikilia hapa nchini.

Miraji ambaye amerejea Simba akitokea Lipuli FC ya mkoani Iringa, amewataka mashabiki wa timu hiyo kwamba wasiwe na wasiwasi na timu yao licha ya ushindani uliopo katika msimu huu.

Akizungumza na gazeti hili jana, baada ya mazoezi ya asubuhi yanayoendelea kwenye viwanja vya Gymkhana, Miraji alisema Ligi Kuu msimu huu ina ushindani ambao umetokana na kila timu kujipanga vizuri ili kujiepusha na janga la kushuka daraja.

"Nitaendelea kujituma ili kuifikisha mbali timu yangu kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, naomba mashabiki wangu wazidi kunipa ushirikiano," alisema mchezaji huyo.

Miraji aliongeza kuwa anatarajia kuongeza umakini na kufuata malekezo kutoka kwa makocha wake kwa sababu bado anahitaji kutimiza ndoto za kwenda kucheza nje ya Tanzania.

"Kikubwa ni kumsikiliza mwalimu kwa makini tunapokuwa mazoezini hiyo ndio itanifanya nizidi kuwa bora zaidi, ndani ya klabu na kwenye Timu ya Taifa," alisema mchezaji huyo.

Aidha, alisema lengo lake ni kuona kipaji chake kinaendelea kuimarika na anaamini hilo linawezekana.

Mshambuliaji huyo sasa ameshafunga mabao sita katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inatarajia kusimama kupisha mashindano ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ambayo yatafanyika kuanzia Desemba 7 hadi 19, mwaka huu jijini Kampala, Uganda.

Habari Kubwa