Asisitiza mafunzo ya watumishi kazini

29Nov 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Asisitiza mafunzo ya watumishi kazini

VYUO vya elimu ya juu na mafunzo ya ufundi vimeshauriwa kuandaa mpango mkakati wa kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma ili kuwaongezea ujuzi na maarifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha DC, Alvera Ndabagoye

Mafunzo hayo yameelezwa kuwa yatawawezesha kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoikabili dunia kwa sasa sambamba na kufanikisha azma ya serikali ya kuutumikia umma.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha DC, Alvera Ndabagoye, katika wa kufunga mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha Uhasibu Arusha, kwa wakuu wa shule na walimu wa fedha.

Mafunzo hayo yalihusiana na saikolojia ya uongozi na usimamizi wa fedha za umma.

Ndabagoye alisema mafunzo kazini ni nyenzo muhimu kwa watumishi kwa kuwa huwaongezea tija na ufanisi kazini pamoja na utendaji kazi wao.

Alisema licha ya watumishi kuwa wameajiriwa kutokana na taaluma zao, bado kuna haja ya kupata mafunzo kazini ambayo yatawaongezea weledi na ufanisi zaidi.

"Serikali inashindwa kumudu kuwapeleka watumishi kwenye mafunzo, kutokana na gharama kubwa zinazopangwa na vyuo kulingana mafunzo yenyewe," alisema Alvera.

"Unakuta chuo kinaandaa mafunzo kwa ajili ya watumishi wa kada mbalimbali lakini gharama kwa mtu mmoja ni laki mbili na kuendelea na ukiangalia halmashauri yetu ina watumishi 8,000 hivyo ni vigumu kumudu gharama," aliongeza.

Mkuu wa IAA, Prof. Eliamani Sedoyeki, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi wa serikali kusimamia vizuri rasilimali za umma.

Aidha, alisema chuo hicho kimeandaa mpango wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wakuu wa shule na walimu wa fedha ili kusimamia matumizi sahihi ya fedha.

"Kumekuwa na tatizo la matumizi mabaya ya fedha kwa shule za serikali pia kutokuwa na wahasibu ambao si wasimamizi wa fedha jambo linalosababisha kusuasua kwa taarifa za utunzaji wa fedha," alisema  Sedoyeka.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Oldonyosambu, Richard Migabuso, alisema mafunzo hayo yatawaongezea maarifa ya usimamizi wa fedha za umma hususani kwenye kipengele cha ulinganifu wa hesabu.

Habari Kubwa