RC amjia juu ofisa wa manunuzi

29Nov 2019
Mary Mosha
SIHA
Nipashe
RC amjia juu ofisa wa manunuzi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amemtaka ofisa manunuzi wa Halmashauri ya Siha, Costantine Nkya, kuandika taarifa ya upungufu wa usimamizi mbovu katika majengo ya hospitali ya wilaya hiyo.

Akizungumza kwenye kikao cha watumishi wa halmashauri sambamba na kumtambulisha katibu tawala wa mkoa huo, Abibu Kazungu.

Alisema awali majengo hayo ya hospitali yangekamilishwa kwa Sh. 1. 5 bilioni, lakini kutokana na usimamizi mbovu inadaiwa  zinahitajika tena nyongeza ya  kiasi cha Sh. 370 milioni kumalizia ujenzi huo.

''Hapa ofisa manunuzi umeshindwa,  mhandisi umeshindwa, kamati imeshindwa… hatuko salama sana, hii hospitali naomba taarifa yako niipate  haraka nijue chakufanya,'' alisema Mghwira.

Mghwira alisema kuwa hospitali hiyo ilitakiwa kukamilisha ujenzi wake mapema mwezi Julai mwaka huu, lakini sasa mwaka unaelekea kumalizika milango na vitasa havijulikani vilipo.

''Nitachukua hatua moja hadi nyingine kuhakikisha hospitali inasimama, na hizi fedha kiasi cha shilingi milioni 370 zinazotakiwa kumalizia ujenzi hazijulikani zitapatikana kwa njia ipi kutokana na uzembe uliojitokeza,'' alisema zaidi Mghwira.

Alisema kitendo cha milango kutengenezewa Dar es Salaam kimechukua muda mrefu kufika kwake licha ya majengo kukamilika jambo ambalo linakwamisha jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya afya.

Habari Kubwa