Miradi nyumba za kuuza izingatie gharama halisi

29Nov 2019
Mhariri
Nipashe
Miradi nyumba za kuuza izingatie gharama halisi

KATIKA kuhakikisha kuwa wananchi wengi wanapata makazi bora na yenye gharama nafuu, serikali imeshusha bei za nyumba za miradi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) nchi nzima kwa karibu-

-asilimia 50 baada ya kubaini zinauzwa kwa gharama kubwa na Watanzania kushindwa kumudu kuzinunua.

Nyumba za vyumba viwili vya kawaida zilizokuwa zinauzwa kwa Sh. milioni 66 zimeshushwa hadi Sh. milioni 36.58 wakati nyumba 169 zenye vyumba vitatu vya kawaida zilizokuwa zinauzwa kwa Sh. million 67.26, Mthamini Mkuu wa Serikali amesema zinaweza kuuzwa kwa Sh. milioni 35 pamoja na kodi ya Sh. 6,300,000, zitauzwa kwa Sh. milioni 41.3.

Pia nyumba 146 zenye vyumba vitatu, viwili vya kawaida na ‘master bedroom’ zilizokuwa zinauzwa Sh. milioni 74.34 zitauzwa hadi Sh. milioni 39 pamoja na kodi ya Sh. 7,020,000 sasa zitauzwa Sh. milioni 46.02.

Nyumba yenye vyumba vitatu na ‘master bedroom’ iliyokuwa inauzwa Sh. milioni 83.78 sasa itanunuliwa kwa Sh. milioni 52 pamoja na kodi ya Sh. 9,360,000 itauzwa kwa Sh. milioni 61.36.

Uamuzi huo ulitangazwa juzi jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Sera, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alipohitimisha kutembelea miradi ya PSSSF.

Mradi huo wenye nyumba za gharama nafuu katika eneo la Buyuni, Chanika una nyumba 480 kati ya hizo 204 hazijapata wanunuzi na 276 malipo yake hayajakamilika.

Waziri alisema mdororo wa ununuzi wa nyumba hizo umesababishwa na makato ya urejeshwaji ya kila mwezi kuwa juu na watumishi wengi kutokumudu bei za nyumba hizo, huku akisema lengo la kujenga nyumba hizo ni kuwauzia watumishi na Watanzania kwa bei nafuu na badala ya kukaa nazo.

Alisema menejimenti ya mfuko iliridhia kutumia Mtathmini Mkuu wa Serikali ili kupata tathmini na thamani halisi ya nyumba hizo kuwa bei halisi na soko lililopo.

Uamuzi wa kushusha bei hiyo kwa nusu ya gharama unaashiria kuwa mchakato kujenga na kuuza nyumba hizo ilikuwa na mapungufu kwa sababu wahusika walipaswa kufanya utafiti wa kina, ikiwamo kuangalia uwezo wa watumishi, wanancni na bei ya soko la nyumba nchini.

Hili linadhihirishwa na Mhagama mwenyewe kwa kueleza kuwa gharama hizo zilikuwa zinawaumiza wananchi, wakati nia ya serikali ni kuwasaidia wananchi wake.

Bila kufanya maandalizi ya kutosha sambamba na utafiti wa kina, miradi ya ujenzi wa nyumba za kuuza itaendelea kuwa mzigo kwa serikali na taasisi zake kwa kuwa nyumba hizo zitakuwa zinajengwa na kukosa wanunuzi kutokana na bei yake kutoendana na uwezo wa watumishi na wananchi kwa ujumla wake.

Kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi bora na kwa gharama nafuu, basi hakuna sababu ya kuzijenga na kuziuza kwa bei ambayo hawataweza kuimudu.

Hata hivyo, suala la makazi bado kina mahitaji makubwa kwa wananchi wengi wanaoishi mijini bila kujali kuwa mhusika mfanyakazi au la, hivyo serikali na taasisi zake bado utekelezaji wa miradi ya nyumba ni fursa ya kuingiza mapato.

Ushauri wetu ni kuwa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuuza kwa watumishi wa serikali na Watanzania kwa ujumla iendelee kutekelezwa, lakini zijengwe nyumba ambazo gharama zake wengi wataweza kuzimudu.

Miradi ya aina hii inaweza kuelekezwa zaidi kwa Jiji la Dodoma ambalo limekuwa makao makuu ya nchi, hivyo kuwa na watumishi wote wa umma na ongezeko zaidi la watu, huku jambo la msingi ilikuwa umakini.

Habari Kubwa