Wataka ulinzi skimu ya umwagiliaji

30Nov 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Wataka ulinzi skimu ya umwagiliaji

WAKULIMA wa mboga  na matunda  katika skimu ya  umwagiliaji ya Lower Moshi, wameiomba serikali kuongeza ulinzi katika usimamizi wa miundombinu  hiyo ili kuleta tija  kwa  Watanzania.

Hayo yalisemwa jana wakati wa ziara ya timu ya wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya ukaguzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Mmoja wa wakulima hao, Severin Msofe, alisema  ni vyema tume kwa kushirikiana na serikali kuanzisha utaratibu maalumu wa kusimamia  miundombinu lengo likiwa kutoharibiwa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

"Tunaomba kutungwe sheria ambayo itawabana wenyeviti wa vijiji, vitongoji na wasimamizi wa skimu hizi kulinda na kutunza miundombinu katika skimu hizi. Wako baadhi ya watu wasio waaminifu  huharibu miundombinu hiyo bila kujali gharama zinazotumika na serikali  kutengeneza," alisema.

Alisema Sheria  ya Umwagiliaji  Na. 5 ya mwaka 2013, inamtaka kila mkulima kulinda miundombinu na atakayekiuka, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Skimu ya Lower Moshi iko umbali wa kilomita tano kutoka Moshi Mjini na ilijengwa mwaka 1984 kwa gharama ya Sh. bilioni tatu kwa ufadhili kati ya serikali ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Aidha, skimu hiyo ni miongoni mwa miundombinu bora ya umwagiliaji nchini ambayo wakulima wake wanalima mpunga kwa wingi na kufuata mwongozo kabambe wa umwagiliaji.

Eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ni zaidi ya hekta 2,000 lakini eneo lililoendelezwa kwa miundombinu bora ya umwagiliaji ni hekta 1,100, sawa na asilimia 55.

Vyanzo vya maji katika skimu hii ni mto na chemchem za Njoro na Mandaka ambazo hupeleka maji kwenye mabanio ya Mabogini na Rau.

Habari Kubwa