Msako wanaokata nyama kwa magogo watangazwa

30Nov 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Msako wanaokata nyama kwa magogo watangazwa

BODI ya Nyama nchini inatarajia kuanza msako wiki ijayo kwa wafanyabiashara wa mabucha ya nyama na samaki wanaotumia magogo kukata nyama.

Imesema msako huo pia utaangazia kundi la wafanyabiashara wanaobeba nyama begani, ikiwaagiza kuzingatia kanuni za usafi katika sehemu za biashara zao ili kujiepuka na magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Kaimu Msajili wa bodi hiyo, Imani Sichalwe, alisema msako huo utajumuisha timu ya bodi na watalaamu wa afya ili kuwachukulia hatua wafanyabiashara wasiozingatia masharti yaliyowekwa kwa wauzaji wa nyama.

"Mfano, suala la ubebaji nyama mgongoni ni hatari kwa afya ya jamii kwa sababu nyama inapogusa migongo ya watu, inasababisha jamii kupata magonjwa yatokanayo na uchafu," alisema.

"Hata makoti wanayovaa wabebaji, baadhi si safi na hivyo kuhatarisha afya za walaji. Hakuna kubeba nyama mgongoni wala kichwani, unapoishusha katika gari la nyama mnapaswa kushikishana mikononi na siyo kujitwisha," alisema.

"Kukatia nyama kwenye magogo ni hatari sana, vijiti huchanganyikana na nyama, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu."

Ofisa Usajili wa bodi hiyo, Godfrey Sosthenes, alisema wauza nyama wote wanapaswa kujisajili ili iwe rahisi kuwatambua katika maeneo wanayofanyia kazi.

"Kuanzia wiki ijayo, tutasajili wafanyabiashara wa mabucha ili kuwatambua idadi yao na kuwaelekeza masharti ya ufanyaji biashara hiyo," alisema.

Habari Kubwa