SMZ yasaka mzabuni kusambaza mchanga

30Nov 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBR
Nipashe
SMZ yasaka mzabuni kusambaza mchanga

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema iko katika mchakato wa kutafuta wakala wa kuuza mchanga kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa kawaida kupata huduma hiyo kwa bei rahisi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk. Makame Ali Ussi, alisema jana wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Magomeni, Rashid Makame Shamsi, aliyetaka kujua utaratibu wa wananchi wa kawaida kupata huduma ya mchanga imefikia wapi hadi sasa.

Alikiri kwamba upatikanaji wa mchanga kwa wananchi wa kawaida umekuwa na changamoto mbalimbali kiasi cha wengi kushindwa kumudu kupata.

Ussi alisema awali wizara ilitayarisha mfumo ambao ni rafiki kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wa kawaida kupata mchanga bila ya usumbufu.

''Mheshimiwa Spika Wizara iko katika mchakato ambao utawawezesha wananchi wa kawaida kupata huduma ya rasilimali ya mchanga bila ya usumbufu,” alisema.

Naibu waziri huyo alisema wizara inachukua kila aina ya tahadhari katika suala la mchanga na kuona kwamba rasilimali hiyo inatumika vizuri kwa faida ya wananchi wote.

Alisema hali ya mchanga Zanzibar si nzuri na kwamba umakini wa matumizi yake unahitajika ili kuwawezesha wananchi wengi kufaidika na rasilimali hiyo.

Alisema hivi sasa baadhi ya miradi ya ujenzi ya serikali imechelewa kumalizika kwa wakati kwa sababu ya ukosefu wa mchanga.

Habari Kubwa